Mkuu wa mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakari Kunenge.
…….
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
VIFO vya uzazi kwa mama Mkoani Pwani vimepungua kutoka vifo 96 kwa mwaka 2018 kati ya akinamama waliofika vituoni 43,488 hadi kufikia vifo 35 kwa mwaka 2022 kati ya akinamama 56,439.
Aidha Vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa asilimia 5.5 kutoka 475 kwa mwaka 2018 na kufikia vifo 390 kwa mwaka 2022.
Hayo yamebainika wakati Mkuu wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge alipokuwa akizindua mpango wa mfumo wa m.mama Mkoani humo , ukumbi wa wauguzi Kibaha Mjini,mfumo ambao utarahisisha masuala ya usafiri wa dharura ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Alieleza licha ya mafanikio na changamoto zilizopo, ujio wa mfumo wa m.mama utaleta matokeo chanya katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Alielekeza kila mmoja kwa nafasi yake akatimize wajibu wake, ili kutekeleza mfumo huo.
“Mfumo huu upewe kipaombele ,Nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa m.mama ,maana inakwenda kunusuru maisha ya mama na mtoto,ni ibada,Twende tukatimize wajibu wetu kufanikisha hili hadi ngazi za chini ,agizo la Rais linahitaji utekelezaji, tutapimana kulingana na utekelezaji,””Naamini Mkoa utafanya vizuri, alisisitiza Kunenge.
Hata hivyo Kunenge alieleza, wakati ikizingumziwa m.mama inatakiwa iende Sambamba na mkakati wa lishe, ili kuleta tija katika kuboresha huduma za afya ya uzazi.
Awali mganga mkuu wa mkoa wa Pwani dkt.Gunini Kamba anaeleza, changamoto kubwa ni jiografia magari ya wagonjwa kutofika kwa wakati mama akipata dharura lakini m.mama itakuwa mkombozi.
Alibainisha vifo vya uzazi kwa mama na mtoto kwenye vituo mbalimbali vimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutoka mwaka 2018-2022.
“Kazi bado ipo,jitihada ziongezeke ili kuendelea kupunguza idadi hii ya vifo,kwani hakuna anaefurahi kupoteza mama ama mtoto wakati wa kujifungua au kabla ya kujifungua ” anasisitiza.
Gunini alisema,lengo ni kuondoa kabisa vifo vya mama na mtoto na kwa ujio wa m.mama malengo hayo watayafikia.
Akitoa taarifa ya Hali Halisi ya viashiria vya huduma za afya ya uzazi mama na mtoto ,Mratibu wa huduma za afya ya uzazi,mama na mtoto Mkoani Pwani, Joyce alieleza utoaji huduma wa dharura umeongezeka kutoka vituo tisa mwaka 2018 ambapo kwa mwaka 2022 vimefikia 23.
Pamoja na hayo alisema kwamba, vituo vya kutolea huduma ya afya vimeongezeka kutoka 300 na Sasa vipo 446.
Alieleza, penye mafanikio hapakosi changamoto,kwani lipo tatizo la udumavu na ukondefu kwani hali ya lishe,inachangia vifo vya uzazi kwa watoto na mama ,ambapo ukondefu umeongezeka .
Alisema, ukondefu umeongezeka kwa asilimia 7.2 kunatokana na ukosefu wa uhakika wa chakula, magonjwa,malezi duni na uelewa mdogo wa lishe bora.
Akielezea kuhusu utekelezaji wa Kitaifa wa huduma ya usafiri wa dharura (m.mama) kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI dkt.Mshana alisema ni mfumo unaolenga kutoa huduma ya usafiri kwa mama na mtoto kupunguza matatizo ya usafiri wakati wa uzazi kwenda rufaa ili kuokoa maisha ya mama na mtoto kijumla.