Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimkaribisha Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Balozi Dkt. Mohamed El Badry katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Balozi Dkt. Mohamed El Badry katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Balozi Dkt. Mohamed El Badry pamoja na Balozi wa Misri Nchini, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Balozi Dkt. Mohamed El Badry pamoja na Balozi wa Misri Nchini, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail katika picha ya pamoja na ujumbe wake.
…..
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kuimarisha ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri katika sekta za biashara na uwekezaji.
Hayo yamebainishwa wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) na Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Balozi Dkt. Mohamed El Badry walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Balozi Mbarouk amesema kuwa ni wakati muafaka kwa Serikali za Tanzania na Misri kuwekeza zaidi katika sekta ya biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa mataifa yote mawili.
“Ili kukuza na kuimarisha misingi ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Misri tunahitaji kufanya mkutano wa Mkutano wa Tume ya pamoja ya Ushirikiano ya Kudumu (JPC) kati ya Tanzania na Misri, pamoja na kuanzisha Baraza la biashara ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara wetu kubadilishana uzoefu na mawazo ya biashara na uwekezaji,” alisema Balozi Mbarouk.
Aidha, Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepanga kufanya Mkutano wa Tume ya pamoja ya Ushirikiano ya Kudumu (JPC) kati ya Tanzania na Misri mwezi Oktoba, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili mazingira ya biashara na uwekezaji kwa pande zote mbili.
“Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kuondoa kero mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wawekezaji hivyo mazingira ya biashara na uwekezaji ni mazuri na yanaridhisha,” aliongeza Balozi Mbarouk.
Naye Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Balozi Dkt. Mohamed El Badry alisema kuwa kufanyika kwa JPC ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa Misri na Tanzania katika sekta ya biashara na uwekezaji.
“tumejadili na kukubaliana kuanzisha Baraza la biashara kati ya nchi zetu ili kuweza kuimarisha sekta hiyo kwa maslahi ya pande zote mbili,” alisema Balozi Badry
Balozi Badry aliongeza kuwa Misri imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, maji, nishati, utamaduni, utalii, kilimo pamoja na uvuvi na mifugo, hivyo ni wakati muafaka kwa mataifa hayo mawili kujikita zaidi katika sekta ya biashara na uwekezaji.