Mashujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), Kata ya Manyoni wakiandamana maandamano ya amani ya kupinga ukatili wa kijinsia, ushoga na usagaji yaliyofanyika mjini Manyoni jana. Maandamano hayo yameandaliwa na SMAUJATA Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), Wilaya ya
Manyoni mkoani Singida wamefanya maandano ya amani ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ushoga na usagaji kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii
iweze kuachana na vitendo hivyo ambavyo vinakiuka maadili ya kitanzania.
Maandamano hayo yalianzia Sheli ya
Ridhiwani, Hospitali ya Wilaya na Majengo ambapo ilitolewa elimu ya kupinga ukatili sanjari na kuchangia damu salama.
Diwani wa Kata ya Manyoni, Saimoni Mapunda akizungumza baada ya kupokea maandamano hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Kemirembe Lwota ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema maandamano hayo ni ya muhimu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wilayani humo.
Alisema maandamano hayo yalioratibiwa na SMAUJATA na kuambatana na zoezi hilo la uchangiaji damu salama lililoongonzwa na Mtaalam wa damu Kucy Kibaja kutoka Hospitali ya Benjamini jijini Dodoma yalilenga kupinga vitendo vya ukatili, ndoa za jinsia moja (ushoga) , usagaji na ukatili wa aina mbalimbali.
Ili kupanua wigo wa mapambano hayo Mapunda aliwataka SMAUJATA kutoka
ofisini na kwenda kwenye mikusanyiko ya watu kutoa elimu ya kupinga ukatili huo wa kijinsia.
“Nawaomba sio kukaa eneo moja bali nendeni walipo wananchi mkatoe
elimu hiyo ya kupinga ukatili tena bila ya kuona aibu na kuelezea kazi
zinazofanywa na SMAUJATA ili wazielewe,” alisema Mapunda.
Mapunda aliipongeza SMAUJATA kwa kazi kubwa wanayoifanya katika wilaya hiyo ambayo siku za hivi karibuni ilichafuka kutokana na kuwepo kwa matukio ya mauaji yakiambatana na ufukuaji wa makaburi.
Mtaalam wa damu salama kutoka Hospitali ya Benjamini Kucy Kibaji alisema suala la uchangiaji wa damu ni la muhimu kwani inasaidia kuwaongezea majeruhi wa ajali, wajawazito wanapojifungua.
Alisema mbali ya kusaidia makundi hayo hivi sasa wanatibu watoto wenye
sikoseli ambao wanatumia damu nyingi kwa kuchukua uroto kutoka kwa watu wa karibu yao ambao wamezaliwa sehemu moja na kuwa changamoto hiyo haipo kabisa.
Alisema watafanikiwa kuwasaidia watu wenye changamoto hiyo kwa jamii
kuchangia damu kwa wingi kwani mtoto mmoja ili kufanyiwa matibabu na kupona anahitaji chupa za damu 40.
Katika kusanyiko hilo mada kubwa iliyotolewa ilikuwa ni kutoa elimu kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia na umuhimu wa jamii kuhusu uchangiaji wa damu.
Watoa mada hao waliongelea kuhusu kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa
kijinsia na mmomonyoko wa maadili katika jamii ambapo waliwaomba, wazazi na walezi kuwa jirani na watoto wao na kusimamia malezi yao wakiwa shuleni na nyumbani kwani imebainika wanaowafanyia ukatili huo wengi wao ni ndugu zao wa karibu.
Walisema ndoa kuvunjika pia kumechangia kwa kiasi kikubwa watoto kukosa matunzo na uangalizi mzuri na kujikuta wakiingia mitaani ambako wanafanyiwa vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kulawitiwa, kubakwa, ndoa za utotoni na mambo mengine mengi.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni katika maandamano hayo, Diwani wa Kata ya Manyoni, Saimon Mapunda, akihutubia baada ya kupokea maandamano hayo.