Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakari Kunenge akizindua Jengo la Zahanati kwenye Kituo cha watoto Yatima Kibaha Children Village Center kilichopo Mtaa wa Simbani Halmashauri ya Mji Kibaha.
………
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakari Kunenge amezindua Jengo la Zahanati kwenye Kituo cha watoto yatima Kibaha Children Village Center kilichopo Mtaa wa Simbani Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kituo hicho kina Jumla ya watoto 16 ambapo kinachoendeshwa na Mwenyekiti wa fursa Sawa kwa wote Mama Anna Mkapa.
Ujenzi wa kituo hicho umegharimu sh. 480 milioni kwa ufadhili wa Balozi wa Heshima wa Tanzania Ujerumani Mhe.Petra Hammelmann kupitia taasisi yake ya Paulchen Esperanza Foundation kwa kushirikiana na Werderhausen Foundation zote za nchini Ujerumani.
Akitoa taarifa kwa Kunenge aliyefika kumwakilisha Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe.Angelah Kairuki,Mama Anna Mkapa amesema Zahanati hiyo itawahudumia wanafunzi na wakazi wa Mtaa wa Simbani zaidi ya 200 .
Alielezea,pia itapunguza adha ya kutembea zaidi ya Kilometa 20 walizotumia awali kufuata huduma za afya mahali pengine.
Alitoa ombi kwa serikali kumwezesha samani,dawa na watumishi ili kuanza kutoa huduma.
Nae Kunenge amempongeza Mama Anna Mkapa na bodi ya wadhamini ya EOTF kwa dhamira yao chanya ya kutoa huduma ya Afya kuunga Mkono Jitihada za Dr.Samia Suluhu Hassan,Rais wa Tanzania na kwamba Serikali pekee yake bila kuungwa Mkono na wadau haiwezi kutoa huduma maeneo yote kwa wakati.
Kunenge amekiri kuyafikisha maombi yote kwa Waziri na ameahidi kuyatafutia ufumbuzi maombi yote yaliyopo ngazi ya Mkoa.
Hata hivyo Kunenge ametoa rai kwa taasisi zote zisizo za kiserikali,sekta binafsi,wadau wa Maendeleo kuwekeza kwenye sekta ya Afya ili kuikwamua jamii kutoka kwenye wimbi la maradhi
Equal Opportunities For All Trust Fund (EOTF) ni taasis isiyo ya Kiserikali iliyoasisiwa 1997 ikiwa na dira ya kutoa fursa Sawa kwa jamii duni hasa kwa wanawake na Vijana kujikomboa kutoka kwenye wimbi la Maradhi,umasikini na Ujinga.