Na Shamimu Nyaki
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaagiza Machifu wote nchini kusimamia mila, desturi na tamaduni katika maeneo yao na kuhakikisha vijana wanaelewa umuhimu kwa kuenzi utamaduni wa Taifa na kuwa na maadili mema.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Juni 13, 2023 katika Viwanja vya Redcross Bujora alipofungua Tamasha la Bulabo lililoandaliwa na Kituo cha Utamaduni wa Wasukuma Bujora ambapo amesisitiza jamii kulinda mazingira kwa kuwa ni utamaduni uliorithishwa tangu vizazi na vizazi pamoja na kusitiza jamii kujivunia lugha, mavazi, vyakula vya asili pamoja na tiba asili.
“Utamaduni ni kivutio cha utalii, ni lazima sekta hizi zifungamane, kuwe na muendelezo wa matamasha mengi katika jamii zetu ili kuvutia watalii wengi kuja kuona na kujifunza utamaduni wetu, na hapa nazikaribisha Sekta Binafsi kuunga mkono Matamasha haya” amesema Mhe. Samia.
Rais Samia, ameagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia upya Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 na kuona kama inaenda sawa na wakati wa sasa ili kama sivyo ifanyiwe marekebisho mapema na haraka iwezekanavyo.
Awali akimkaribisha Mhe. Rais Samia, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Tamasha hilo linahudhuriwa na washiriki takriban 7,000 kutoka mikoa mbalimbali na litajumuisha ngoma za asili, maonesho ya utamaduni na elimu ya ukatili wa kijinsia.
Mhe. Pindi ameongeza kuwa, Wizara inaendelea kuratibu matamasha mbalimbali ikiwemo Tamasha la Muziki la Cigogo Dodoma, Tamasha la Kuchekea la Mkoa wa Lindi, Tamasha la Kizimkazi Dimbani Zanzibar, Tamasha la Ngoma za Asili linaloratibiwa na Tulia Trust mkoani Mbeya na mengine mengi.
Naye Mkurugenzi wa Makumbusho ya Bujora, Padri Anania Mukanzabi amesema lengo la Tamasha hilo lililoanzishwa Sumve Wilaya ya Kwimba mwaka 1940 ni kufanya sherehe za kumshukuru Mungu kwa mavuno mapya, ambapo amesema Tamasha hilo limeendelea kufanyika kila mwaka.