Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja  Jenerali  Charles Mbuge  akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida. 

Na Mwandishi WetuSingida 

Serikali
kupitia  Ofisi  ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuimarisha
ushirikiano na sekta mbalimbali katika kukabiliana na maafa ili kuhakikisha
wananchi wanaishi katika mazingira salama.

Kauli hiyo imetolewa   mkoani Singida na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti
ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja
Jenerali  Charles Mbuge  wakati akifungua kikao kazi cha Watalam
waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja.

Meja Jenerali Mbuge amesema kumekuwa na ongezeko kubwa
la mwingiliano wa binadamu, wanyama na mazingira ambao  husababisha
kutokea kwa magonjwa mbalimbali yanayotoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu hivyo ipo haja ya   kuwepo kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana  na majanga hayo.

“Tunahuisha mwongozo huu kwa sababu ya mabadiliko
ya sheria na kanuni za usimamizi wa Maafa.

Mwongozo huu ni muhimu katika kurahisisha ushirikiano wa kisekta ili
kujenga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya milipuko ya magonjwa na
dharura zingine zenye madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa husisitiza yakiwemo  Shirika
la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO),  Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Wanyama (WOAH) na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa pamoja husisitiza ushirikiano wa sekta mbalimbali ili  kuwa na mikakati na sera za  pamoja katika kuimarisha afya ya wanadamu,
wanyama na mazingira.

“Ili kutekeleza dhana ya Afya moja, ni muhimu kuwa na miongozo mbalimbali ili kurahishisha uratibu na utendaji katika ngazi zote.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru FAO ambao walianzisha mchakato wa kutengeneza mwongozo huu ambao katika kikao hiki utauhuishwa na kutafsiriwa,” ameeleza. 

Aidha amebainisha kuwa   Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti
ya Maafa ina  wajibu wa kuratibu
utekelezaji wa dhana ya  Afya Moja kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya 2004, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na Mkakati wa Afya Moja 2022-2027.

Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Valentina Sanga akiwasilisha Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja . 

Mtaalam wa Afya ya Jamii kutoka Shirika la Afya Duniani Bi. Pelagia Muchuruza akieleza jambo wakati wa kikao hicho. 

Afisa Kiungo wa Afya Moja kutoka Wizara ya Mifugo
na Uvuvi Dkt. Justine Assenga akifafanua jambo katika kikao hicho.

 Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja  Jenerali  Charles Mbuge 
(katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watalam
waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.

Baadhi ya Wataalam kutoka sekta mbalimbali wakifuatilia kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.