*TARURA yapongezwa kwa ubunifu huo ambao unapunguza gharama

‎Igunga, Tabora

‎Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda amezindua daraja la mawe la Nyandekwa (Arch Bridge) lenye urefu wa mita 25.5 lililopo kwenye barabara ya Nyandekwa–Mwabubele wilayani Igunga mkoani Tabora. 

Akizindua daraja hilo Ndugu Wazo ameipongeza TARURA kwa ubunifu huo na kuongeza kwamba ujenzi umeweza kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.

‎Akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA wilaya ya Igunga Mhandisi Aswile Mwasaga amesema kuwa mradi huo umegharimu shilingi milioni 203.86 ukifadhiliwa na Serikali Kuu kupitia Fedha za Maendeleo za Tozo ya Mafuta na umekamilika kwa asilimia 100.

‎Daraja hilo linatarajiwa kuboresha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa kata za Nyandekwa na Ntobo zenye vijiji saba (7) na wakazi 24,902 pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa kwa kipindi chote cha mwaka.

‎Naye, mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mwakipanga Leticia Clement ameishukuru serikali kwa kuwajengea daraja hilo ambalo limewasaidia kufika shuleni bila changamoto kwani kabla ya daraja hilo kipindi cha masika walikuwa wakipata shida kuvuka kwenda shuleni kutokana na na maji kujaa na kushindwa kuvuka mto.

‎Bw. Hamisi Makala mkazi wa Nyandekwa amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi walikuwa wakipata shida ya usafiri hasa wajawazito walishindwa kwenda kujifungua lakini sasa wananchi wananufaika na daraja hilo kwani wanafikia huduma za kijamii na kiuchumi kwa urahisi.