Benki ya NMB ikiwa inaendeea kusherehekea safari yake ya mafanikio ya miaka 25, Iliandaa bonanza la Michezo waliloliita Vuta Nikuvute visiwani Zanzibar.
Kikosi cha timu ya mpira wa miguu cha Benki ya NMB, kilitawazwa mabingwa wa tamasha la michezo la kudumisha ushirikiano baina ya benki hiyo na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, Visiwani Zanzibar.
Shujaa wa timu ya NMB inayonolewa na nyota wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mohammed Hussein ‘Mmachinga,’ alikuwa ni mshambuliaji Simon Zubeir, aliyetikisa nyavu mara tatu ‘hat trick,’ mabao yote akiyafunga kipindi cha pili, baada ya dakika 45 za kwanza kumalizika kwa sare tasa, huku kila upande ukionesha kiwango bora.
Bonanza hilo lilitanguliwa na matembezi ya hisani yaliyoshirikisha wafanyakazi wa NMB, Wajumbe wa Baraza la Mawaziri Zanzibar wachezaji wa timu za michezo yote na kikundi cha mbio za taratibu ‘jogging’ cha Island Exercise Club, huku washiriki wote wakiongozwa na Mgeni Rasmi, Zubeir Ali Maulid, ambaye ni Spika wa Baraza la Mawaziri Zanzibar pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB – Ruth Zaipuna.Bonanza hili lilijumuisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa kikapu, netiboli, kuvuta kamba, mbio fupi za mita 100, mbio za magunia na kufukuza kuku, ambako ukiondoa soka, NMB pia ilitwaa ubingwa kuvuta kamba (wanawake), mbio za mita 100 (wanaume).
Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, timu zake zilitwaa ubingwa katika mchezo ya kikapu (wanaume) walikoshinda pointi 53-42, netiboli (wanawake) magoli 36-21, mbio za magunia wanaume, kuvuta kamba (wanaume) na mbio za mita 100 (wanawake).Akizungumza viwanjani hapo, Bi. Ruth, alimuahidi Spika wa Baraza la Wawakilishi kuwa, NMB itaendelea kutoa mchango wa kustawisha sekta ya michezo visiwani Zanzibar, kwani anamini michezo ni afya.