Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema katika Mtaala mpya wa masomo kwa ngazi zote za Elimu nchini, Michezo na Sanaa imekuwa somo la kufundishwa shuleni na lipo pia katika tahasusi za kidato cha tano hadi chuo Kikuu.
Mhe. Mwinjuma amesema hayo Juni 10, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya kidato cha IV na VI ya Shule ya Academic International Secondary School, ambapo amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya Elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza miundombinu na kuboresha iliyopo.
“Elimu ni ufunguo wa maisha, lakini pia Sanaa, Utamaduni na Michezo ni Sekta ambazo katika dunia la leo zina mchango mkubwa katika ajira na kujitegemea, hivyo ni lazima tutoe nafasi kwa watoto wetu kujishughulisha na sekta hizi” amesisitiza Mhe. Mwinjuma.
Aidha, ametoa wito kwa shule binafsi nchini kushiriki katika michezo ya UMITASHUMTA na UMISSSETA kama ambavyo Shule za Serikali zinavyoshiriki.