Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same,Ndg. Abdillahi Mnyambwa amewapongeza wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini(TARURA)Wilaya ya Same kwa kukamilisha Miradi mbalimbali Wilayani humo kwa wakati na kwa ubora.
Mwenyekiti huyo alitoa pongezi hizo wakati Kamati ya Siasa ya Wilaya ilipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi (2020-2025) ya CCM ambapo walitembelea ujenzi wa Daraja la mawe lililopo Kata ya Kalemawe na ukarabati wa kiwango cha zege wa mita 810 za eneo korofi katika barabara ya Hedaru-Vunta-Myamba.
Akitoa taarifa ya Ujenzi wa daraja la mawe Meneja wa TARURA Wilaya ya Same Mhandisi James Mnene alisema daraja hilo limejengwa kwa Tsh.mil 239 na limekamilika kwa asilimia 98.
“Daraja hilo lina urefu wa mita 36 na upana wa mita tisa na lina uwezo wa kubeba tani 37 bila wasiwasi pia umri wake wa kutumika ni miaka 100″alisema Mnene.
Kwa upande wa ujenzi wa maeneo korofi ya Barabara ya Hedaru-Vunta-Myamba Mhandisi huyo alisema eneo korofi lenye urefu wa mita 810 linajengwa kwa kiwango cha zege na gharama za ujenzi huo ni Tsh.655.5 mil.
Mhandisi Mnene alisema Miradi yote hiyo inatarajia kukamilika mwaka huu wa fedha.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Anastazia Tutuba amesema ukarabati wa Barabara na Ujenzi wa madaraja unarahisisha usafirishaji wa vifaa katika Ujenzi wa Miradi mbalimba inayotekelezwa Wilayani humo.
Aisha alisema ukarabati huo unachangia ongezeko la mapato ya Halmashauri ambapo wafanyabiashara hupata urahisi wa kusafirisha mazao na hivyo kuchangia mapato ya Halmashauri.
Katika Ziara hiyo Kamati ya siasa ilitembelea Miradi ujenzi wa daraja la mawe,ujenzi wa eneo korofi barabara ya Hedaru-Vunta-Myamba,ujenzi wa Barabara ya Maore-Mpirani-Ndungu.
Miradi mingine iliyotembelewa ni Mradi wa maji Mabilioni -Hedaru,ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na Ukarabati wa mabweni mawili shule ya Sekondari Same.