Mgombea wa Urais Shirikisho la Filamu nchini Tanzania (TAFF) Dkt. David Msuya akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 10/6/2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Shirikisho hilo.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mgombea wa Urais Shirikisho la Filamu nchini Tanzania Dkt. David Msuya amewataka baadhi ya wasanii wa Bongo Movie kuacha tabia kuchafuana, kwenda kinyume na taratibu jambo ambalo linaweza kuvuruga uchaguzi wa shirikisho hilo.
Kauli ya Dkt. Msuya imekuja baada Serikali kuhairisha uchaguzi wa Shirikisho la Filamu nchini kwa kile kinachodaiwa baadhi ya watu kwenda kuongea na viongozi wenye dhamana kuhusu uchaguzi bila kufata utaratibu na kanuni.
Akizungumza leo tarehe 10/6/2023 Jijini Dar es Salaam, Mgombea wa Urais Shirikisho la Filamu Tanzania Dkt. Msuya, amesema kuwa wakati umefika wasanii kuongea lugha moja kutokana Serikali ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani bado ina nia njema katika kuhakikisha wasanii wa filamu wanafanikiwa.
Dkt. Msuya amesema kuna baadhi ya wasanii wamekuwa wakitumia vibaya ukaribu wao na viongozi serikali jambo ambalo linasababisha kubadilishwa utaratibu ambao haupo katika kanuni.
Amesema kuwa Shirikisho la Filamu ni shirikisho huru ambalo haliwezi kuingiliwa na mamlaka yoyote katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Serikali inatakiwa kupokea mgombea aliyepitishwa na shirikisho, lakini leo wakisimamisha uchaguzi kwa sababu za watu binafsi hakuna faida yoyote na wanaendelea kuwagawa wasanii wa filamu nchini” amesema Dkt. Msuya.
Amefafanua kuwa wapo baadhi ya watu wamesafiri kutoka Mkoa wa Dar es Salaam kwenda Dodoma kuonana na viongozi wa serikali ili kukwamisha uchaguzi.
Dkt. Msuya amesema kuwa watu waliokwenda kuonana na viongozi wa serikali bila kufata utaratibu sio jambo njema kutokana linaleta shida katika kufanikisha majukumu ya Shirikisho.
“Naiomba baadhi ya viongozi wa serikali waache kukombatia kikundi cha wasanii, wafate utaratibu na kanuni jambo ambalo litaleta tija kwa Taifa” amesema Dkt. Msuya
Ameeleza kuwa Waziri mwenye dhamana anapaswa kuwa makini katika kuhakikisha anawaunganisha wasanii wa Bongo Movie kwa kuweka utaratibu rafiki katika utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia kanuni na taratibu.
Dkt. Msuya amesikitishwa na uwepo wa baadhi ya wasanii ambao wamekuwa wapiga debe na sio wapiga, huku wakiendelea kuwagawa wasanii katika shirikisho hilo.
Msomi huyo amesema kuwa Tanzania bado kuna changamoto ya usambazaji wa kazi za wasanii, hivyo lengo lake ni kuleta wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kukuza soko la filamu nchini.