Na John Walter-Manyara
Kampuni ya mbegu ya ZAMSEED imewashauri wakulima kuacha kufanya Kilimo cha Mazoea ili kupata mavuno Mengi.
Akizungumza na wakulima wa kata ya Nangwa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara afisa masoko wa Kampuni ya ZAMSEED Kanda ya kati na kaskazini William Massey, amesema baadhi ya wakulima wanashindwa kupata mavuno ya kutosha kutokana na kupanda aina nyingi ya mazao kwenye shamba Moja na mwishowe kuishia kulalamika.
Massey amewahakikishia wakulima wa wilaya ya Hanang’ na mkoa wa Manyara kwa ujumla kuwa wataendelea kutoa mbegu kwa ubora unaotakiwa na zenye kutoa matokeo chanya.
Afisa Kilimo wilaya ya Hanang’ Liberatus Msasa amesema ni muhimu kuchanganya mazao kwa kufuata kanuni za Kilimo kwa kuacha nafasi mmea kwa mmea ili kutoa fursa kwa mazao kupata mwanga wa kutosha na kuzalisha ili kupata mavuno mengi yatakayomwezesha mkulima kupata chakula na hata kwa biashara.
Msasa amesema Mbegu za ZAMSEED ni rafiki wa mkulima kwa kuwa inatoa mavuno ya kutosha endapo mkulima atazingatia ushauri wa Wataalamu na matumizi sahihi ya mbolea.
“Si kila mbegu itaweza kufanya vizuri kila mahali, inategemea aina ya udongo uliopo, hali ya hewa, kwa hiyo niwashukuru ZAMSEED kwa hii teknolojia waliyokuja nayo mpya na utaratibu wa kuwapa mafunzo wakulima kabla ya msimu na baada ya msimu wa kilimo, wanatusaidia sana sisi kama serikali” alisema Msasa
Msisitizo huo wa kutumia mbegu bora za mahindi ulioofanyika katika kata ya Nangwa wilaya ya Hanang’ umeenda sambamba na mafunzo ya kilimo bora.
Aidha wakulima walioneshwa kwa vitendo mashamba darasa ambayo yamepandwa mbegu za ZAMSEED ambazo zimezaa vizuri.
Nao baadhi ya wakulima ambao wameshatumia mbegu hizo wamekiri kufanya vizuri na kwamba mavuno yao yameongezeka Zaidi tofauti na miaka ya nyuma licha ya kuwepo kwa ukame katika msimu huu.