Na. WAF – Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu mapema leo ameagana na aliyekuwa Mwalikishi Mkazi Kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Zabron Yoti na kumkaribisha Mwakilishi mpya wa Shirika hilo nchini Tanzania Dkt. Charles Sagoe-Moses
Waziri Ummy amemshukuru Dkt. Yoti kwa ushirikiano wake alioutoa katika kipindi chake ambacho amelitumikia Shirika hilo na kumtakia heri katika safari yake ya kuwatumikia na kuwasaidia watu.
“Nakushukuru sana Kaka Yoti kwa pamoja tumeweza kushirikiana hasa katika kuumaliza ugonjwa wa Marbug uliotokea katika Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera kwakweli hukurudi nyuma tulikua pamoja mwanzo hadi mwisho nakushukuru sana.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Katika kikao hicho kifupi Waziri Ummy amemkaribisha Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Charles Sagoe-Moses na kumweleza changamoto katika sekta ya afya akigusia magonjwa yakuambukiza na magonjwa yasiyoambukiza.
“Karibu sana Dkt. Charles tuna changamoto nyingi katika sekta ya afya hasa kwa magonjwa yakuambukiza na magonjwa yasiyoambukiza kwa kweli tunahitaji kuweka nguvu kwa kupata wataalam zaidi wenye weledi wa kutosha kwenye eneo hili.” Amesema Waziri Ummy
Pia, Waziri Ummy amepongeza juhudi na mchango wa WHO katika mapambano dhidi ya magonjwa ya milipuko ikiwemo UVIKO -19 na Ugonjwa wa Marburg ambapo kupitia ushirikiano huo Madaktari waliweza kujitoa kwa uzalendo hadi kumalizika kwa ugonjwa wa Marburg bila kukimbia.
Kwa upande wake Mwakilishi wa (WHO) nchini Tanzania Dkt. Charles ameahidi kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake Dkt. Yoti kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa Sekta ya Afya nchini hasa utoaji wa huduma bora.
“Mhe. Waziri nashukuru sana kwa kunikaribisha, nimefurahi kukutana nawe naahidi nitaendelea kutoa ushirikiano na Nipo hapa kukusaidia ili kufikia malengo ya Wizara na kuwasaidia Watanzania katika kuboresha huduma za afya nchini.” Amesema Dkt. Sagoe-Moses