………………….
Wizara ya Maliasili na Utalii imepongezwa kwa kuzishirikisha Serikali za mitaa, Viongozi wa dini na wananchi katika uhifadhi wa maeneo ya Malikale yanayohifadhiwa kisheria nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule kwenye kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Uongozi wa Wilaya ya Kinondoni, Viongozi wa Dini, kamati ya Usalama wilaya ya Kinondoni na Wananchi juu ya Uhifadhi endelevu wa eneo la Magofu ya Kunduchi.
Akiendesha kikao kazi hicho Jijini Dar es Salaam, Mhe. Mtambule ameishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia namna ya kuwashirikisha wakazi wanaozunguka maeneo ya Malikale ili watambue umuhimu wa maeneo hayo kiuhifadhi na kiutalii.
Mhe. Mtambule ameongeza kuwa kwa kujifunza umuhimu wa uhifadhi wa maeneo ya Malikale Wakazi wa Kinondoni wanaoishi jirani na maeneo ya malikale watapata uelewa na uzoefu wa kujifunza kutoka kwenye maeneo mengine ya kihistoria ikiwemo Kilwa Mkoani Lindi, Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Mikindani Mkoani Mtwara na Zanzibar kuona namna Wananchi wanavyoshiriki katika Uhifadhi, na Utalii endelevu Kwa faida ya kizazi cha Sasa na Kijacho.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Christowaja Ntandu amesema Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa imejipanga vyema katika kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika Shughuli za Uhifadhi na Utangazaji wa maeneo yaliyohifadhiwa ili yaweze kudumu na kuvutia Watalii wengi zaidi na kuongeza pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja.
Dkt. Ntandu ameongeza kuwa, Ushirikishwaji wa wananchi na wadau wengine kwenye Uhifadhi wa Maeneo ya Malikale ni moja ya mikakati ya Idara hiyo.
Naye Katibu wa BAKWATA Kunduchi Bw. Suleiman Nassoro, ameihakikishia Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana vyema katika Uhifadhi endelevu wa maeneo ya Malikale na kuipongeza Wizara hiyo Kwa kuona Umuhimu wa kutoa uelewa wa pamoja na kushirikiana na Wadau hususani wanaoishi jirani na maeneo hayo.
Kikao kazi hicho kilichofanyika kwenye eneo la Malikale la Kunduchi Jijini Dar es Salaam, kimeudhuriwa na Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni ndugu Stella Msofe, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kinondoni, Viongozi wadini, Maafisa Waandamizi wa Halmashauri ya Kinondoni na Maafisa Waandamizi wa Idara ya Malikale pamoja na Wadau mbalimbali.
Wilaya ya Kinondoni ina maeneo mbalimbali ya Malikale hususani eneo lenye historia adhimu na adimu la Kunduchi lililopo kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi maeneo mengine yenye historia ya upekee huo ni pamoja na Mbwa Maji Kigamboni, Kaole Bagamoyo, Kilwa Kisiwani na Songomnara, Mikindani Mtwara.