Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dodoma
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na watumishi wa Wizara hiyo na kuwasisitiza kufanya kazi kwa weledi ili kufikia malengo ya Serikali.
Kikao hicho kimefanyika Juni 08, 2023 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambacho kilihusisha Menejimenti pamoja na watumishi wa Wizara hiyo.
Balozi Dkt. Chana amesema sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ni muhimu kwa Taifa na ustawi wa afya ya watanzania ndiyo maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa na mchango mkubwa na yupo bega kwa bega na wizara hiyo ili kuhakikisha inawasaidia Watanzania.
Akifunga kikao hicho, kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma amewahimiza watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuwa na mipango madhubuti ya utekelezaji ili kuifanya kazi iwe rahisi na kumsaidia Rais kwenye sekta hizo.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wizara amesema kuwa, sekta za Wizara hiyo katika Mtaala mpya wa masomo kwa ngazi zote za Elimu nchini imepewa kipaumbele na sasa Michezo na Sanaa imekuwa somo la kufundishwa shuleni kama somo na lipo pia katika tahasusi za kidato cha tano hadi chuo Kikuu.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Bw. Nicholas Mkapa, Wajumbe wa Menejimenti pamoja na watumishi ambapo vikao vya aina hiyo vitakuwa vinafanyika mara nne kwa mwaka.