NA WAF- BUNGENI DODOMA
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2022-2023, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga zaidi ya Milioni 725 kwaajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa tatu wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza nchini.
Dkt. Mollel amesema hayo, leo Juni 7, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Bernabetha Kasabago Mushashu katika Bunge la kumi na mbili Mkutano wa kumi na moja kikao cha 42, Jijini Dodoma.
Amesema, “katika mwaka wa fedha 2022-2023, Serikali Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 725 kwaajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa tatu wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza 2021-2026 nchini, huku mikakati mahususi ya udhibiti visababishi vya magonjwa hayo yasiyoambukiza.”
Ameendelea kusema, Serikali imeweka mikakati thabiti ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kuimarisha ushirikishwaji wa Sekta mtambuka, kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma, kuwajengea uwezo watumishi ili kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha na kusimamia shughuli za utafiti na kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia za kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa elimu juu ya njia za kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kuzingatia kanuni bora za lishe, kupunguza unywaji wa pombe uliopitiliza na matumizi ya mafuta mengi kwenye vyakula.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Serikali ya Rais Samia imeweka fedha nyingi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo eneo la manunuzi ya vifaa tiba ikiwemo CT-SCAN katika kila hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja kusaini mikakati kwa Wakuu wa Mikoa wote kuhusu masuala ya lishe kwenye kila mkoa.
Kwa upande mwingine, Dkt. Mollel amesema Mkakati mwingine wa mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ni kuunga mkono kwa Mpango wa Bima ya Afya kwa wote pindi utapoletwa Bungeni ili kumpa haki kila mwananchi kupata matibabu bila malipo kuanzia ngazi ya Zahanati hadi hospitali ya Taifa.
Pia, Dkt. Mollel amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuongeza kasi kwenye eneo la upatikanaji wa dawa katika zahanati na vituo vya afya, idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya Zahanati imeongezeka kutoka aina 254 mwaka 2015 hadi kufikia aina 451 mwaka 2023, huku ngazi ya Kituo cha Afya ikiongezeka kutoka aina 414 mwaka 2015 hadi kufikia aina 828 mwaka 2023.