Mkurugenzi Idara ya Mafunzo na Elimu ya Lishe, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Esther Nkuba akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 7/6/2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu Siku ya Chakula Salama Duniani.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imeitaka jamii kula chakula vyenye virutubisho kwa ajili ya kujenga afya pamoja na kujikinga na magonjwa yanayosababishwa na ulaji wa vyakula ambavyo haviko salama.
Akizungumza leo tarehe 7/6/2023 Jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Chakula Salama Duniani, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mafunzo na Elimu ya Lishe TFNC, Dkt. Esther Nkuba, amesema kuwa ulaji wa chakula salama ni muhimu kwa ajili ya afya ya binadamu na kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Dkt. Nkuba amesema kuwa duniani inakadiriwa watu milioni 600 wanapata magonjwa yanatokana na kula chakula ambacho sio salama, huku asilimia 40 wakiwa watoto chini ya miaka mitano.
Amesema kuwa pia watu 420,000 wanafariki dunia kutokana na madhara ya kula chakula ambacho sio salama kwa afya ya binadamu.
“Chakula salama maandalizi yake kuanzia shambani wakati analima na kuvuna, anatumia mbinu za kitaalamu ? anavunaje mazao ? na anakwenda kuifadhi wapi ? ” amesema Dkt. Nkuba
Amesema ni jukumu la kila mtu kusimamia Uzalishaji wa chukula ikiwemo msafirishaji, watumiaji ili kuepukana na magonjwa yanayoweza kukingika.
Dkt. Nkuba amesema kuwa ni vizuri mpishi azingatie usafi na usalama wakati anaandaa chakula ni jambo la muhimu kwa afya ya binadamu.
Amesema kuwa usafi ni muhimu sana kwani kuna magonjwa mengi ambayo yanatokana na ulaji wa chakula ambacho sio salama.
“Magonjwa yanayotokana na kula chakula ambacho sio salama yanamadhara makubwa kiafya pamoja na uchumi wa nchi” amesema Dkt. Nkuba.
Amesema kuwa kila mtu au Taasisi inatakiwa kusimama katika sehemu yake ili kuhakikisha tunaondokana na magonjwa yanayotokana na kula chakula ambacho sio salama.
Siku ya Chakula Salama Duniani ilianza mwaka 2018 ambapo siku hiyo imelenga kuweka uwelewa ndani ya watu kuhusu umuhimu wa usalama wa chakula pamoja na kuleta hamasa kwa Mamlaka husika kuchukua hatua juu magonjwa yanayotokana na chakula, huku akieleza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu : Viwango vya Vyakula Huokoa Maisha.