Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeibuka kidedea
na kutunukiwa Tuzo katika maonyesho ya 10 ya Biashara na Utalii yaliyofanyika jijini Tanga kuanzia Mei 28 hadi Juni 6, 2023.
Ushindi huo ambao TANAPA imeupata unatokana na kutoa elimu ya uhifadhi na utalii ikiwa ni huduma ambayo huitoa kwa watalii wa ndani na wa kimataifa ambao wameendeleo kuongezeka katika hifadhi za taifa. Tuzo hii imeliheshimisha shirika na kutoa hamasa ya kuendelea kutoa huduma bora na zenye viwango vya kimataifa.
TANAPA imepata tuzo hiyo kwa kunadi vyema vivutio vyake vilivyomo katika hifadhi za taifa 22.
Maonesho haya ya Biashara na Utalii yaliyobebwa na kaulimbiu “Kilimo, Viwanda, Utalii na Madini ndio msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi” yaliyoandaliwa na Tanzania Chamber of Commerce, hufanyika kila mwaka mkoani Tanga katika viwanja vya Mwahako yakijumuisha makampuni, taasisi za serikali na zisizo za kiserikali.