NA MWANDISHI WETU, NJOMBE
Serikali ya Tanzania imeanza kulipa fidia kiasi cha bil 15.4 kwa wanufaika 1,142 waliyopisha miradi ya chuma cha Liganga na mkaa wa Mawe Mchuchumana wilayani Ludewa na kisha kuwahakikishia wakazi wa Ludewa na Tanzania kwa ujumla kuanza machimbo baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.
Akizungumza kwa njia ya simu katika mkutano uliyokutanisha wanufaika wa fidia ,taasisi za fedha ,wawakilishi wa sekta binafsi na maofisa kutosha wa shirika la maendeleo ya taifa NDC,Serikali ya mkoa wa Njombe na Waziri wa Biashara Viwanda na Uwekezaji Dkt Ashatu Kijaji baada ya kumpigia simu Waziri,Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema serikali imedhamiria kuanza utekelezaji wa mradi huo ambao aliahidi kipindi cha kampeni,
Dkt Samia amesema punde baada ya kukamilisha zoezi la ulipaji wa fidia serikali itakwenda kuanza uchimbaji kwasababu kuanza machimbo hayo kunakwenda kutengeneza fursa nyingi kwa wakazi wa Ludewa,Njombe na Taifa kwa ujumla kwani taifa litaingiza fedha nyingi za kigeni ,kuongeza mapato ya serikali sambamba na kutengeneza ajira nyingi kwa vijana.
Awali akifafanua kuhusu mradi huo mkurugenzi mtendaji wa shirika la maendeleo ya taifa nchini Dkt Nicolaus Shombe amesema mwaka 2007 serikali kupitia baraza la mawaziri ililielekeza shirika la NDC kuwekeza zaidi katika mradi wa chuma na mkaa wa Mawena kisha kuanza kuwekeza kwa mara ya kwanza 2013 ambapo zaidi ya tani mil 428 za mkaa wa mawe huku kwenye chuma kukiwa na tani mil 126 ambacho kinaweza kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 56.
Kuhusu hatua iliyofikiwa na serikali hadi sasa katika ulipaji fidia Dkt Shombe amesema hadi kufika juni 6 wanufaika 39 walikuwa wameanza kulipwa fedha za fidia kwenye akaunti zao na kisha waomba wananchi kutumia vizuri fedha hizo pindi watakapopokea fedha.
Wakati serikali ikonya juu ya matumizi mabovu ya fedha hizo ,Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amewataka wanufaika wote kuanza kufikiria namna ya kuwekeza miradi ya maendeleo hususani nyumba za kulala wageni, kulima vyakula vya kutosha kwa ajili ya kulisha maelfu ya watu katika migodi hiyo na kisha kutoa agizo kwa serikali ya wilaya ya Ludewa kufanya upimaji wa maeneo yote muhimu ya wilaya hiyo ukiwemo mji wa Ludewa.
Katika hatua nyingine Mtaka ameonya wanufaika ambao watatumia fedha vibaya ikiwa ni pamoja na kuwa chanzo cha familia kuvunjika na kudai kwamba wanufaika wa TASAF ambao ni miongoni mwa wanufaika wa fidia hizo watumie fedha vyema kwani baada ya muda mfupi baadae watapaswa kuondolewa kwenye mpango huo wa kunusuru kaya masikini nchini.
Kwa upande wake waziri wa biashara ,viwanda na uwekezaji nchini Dkt Ashatu Kijaji wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo la ulipaji wa fidia amesema mradi huo unakwenda kufanya mapinduzi makubwa kiuchumi kwa wakazi wa Ludewe na taifa la Tanzania kwani utaongeza pato la taifa kwa kupata fedha nyingi za kigeni na kisha kuokoa zaidi ya dolla bil 1 ambazo hutumika na serikali kuagiza chuma nje ya nchi kila mwaka.
Dkt Kijaji amesema kitendo kilichofanywa na rais Samia kutoa bil 15.4 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wakazi wa Mundindi ,Amani na Mkomang’ombe kinakwenda kuandika historia ya milele kwa taifa la Tanzania na kwamba utekelezaji wa jambo hilo umetokana na ahadi yake kipindi cha Kampeni 2020 akiwa wilayani humo.
Ili kuhakikisha fedha za wanufaika wa fidia zinakuwa salama serikali imetumia taasisi za fedha ikiwemo NMB kulipa fedha za fidia wananchi ambapo Vicky Bishubo mkuu wa idara ya huduma za serikali NMB Makao makuu na Straton Chilongoji meneja wa NMB kanda ya Nyanda za juu wamesema hadi kufika juni 7 benki hiyo ilikuwa imefungua akaunti za wananchi kwa asilimia 73 na kisha kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wanufaika ili wasitumie vibaya.
Maofisa hao wamemesema wamejipanga vyema kushirikiana na serikali kuifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa ili wanufaika wanufaike na fidia hizo ili serikali ifikie lengo ililojiwekea katika migodi ya liganga na mchuchuma wilayani Ludewa
Nao baadhi ya wanufaika wa fidia hizo akiwemo Fesi Muhagama wanasema limekuwa ni jambo la kumshukuru mungu kulipwa fidia ya kupisha maeneo yao kwasababu vizazi na vizazi vimepoteza maisha wakati vikisubiri fidia hiyo na kwamba wanakwenda kujipanda ili kutumia fedha hizo kwa tija ya familia zao.