Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Misango, akitoa mada kuhusu mapitio ya maendeleo ya uchumi nchini na fedha za kigeni wakati wa kikao kazi kati ya Benki Kuu ya Tanzania BoT na Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF kilichofanyika leo Juni 6,2023 katika ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Misango, akijibu maswali kadhaa kutoka kwa wahariri kuhusu mapitio ya maendeleo ya uchumi nchini na fedha za kigeni wakati wa kikao kazi kati ya Benki Kuu ya Tanzania BoT na Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF kilichofanyika leo Juni 6,2023 katika ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Idara ya Itifaki na Uhusiano Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Bi. Vick Msina akifafanuabaadhi ya mambo kwa wahariri kuhusu mapitio ya maendeleo ya uchumi nchini na fedha za kigeni wakati wa kikao kazi kati ya Benki Kuu ya Tanzania BoT na Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF kilichofanyika leo Juni 6,2023 katika ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wataalamkutoka Benki Kuu ya Tanzania BoT wakiwa katika kikao hicho.
Pichambalimbali zikiwaonesha baadhi ya wahariri wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa kuhusu mwenendo wa uchumi na fedha za kigeni.
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Tarehe 6/6/2023
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuongeza ukwasi wa dola pamoja na kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya Nchi ili kukabiliana na mwenendo wa uchumi wa Duniani ambao umesababisha bei za bidhaa katika soko la dunia kupanda.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika semina na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa uchumi na Fedha za kigeni, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Dkt. Suleiman Misango, amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya uchumi wa dunia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuongeza ukwasi wa dola katika uchumi.
Dkt. Misango amesema kuwa mwenendo wa uchumi wa dunia umesababisha bei za bidhaa katika soko la dunia zipande na kupelekea mahitaji ya fedha za kigeni kuongezeka.
“Baada ya kupanda kwa bei za bidhaa katika soko la dunia tumuona Benki Kuu nyingi hasa katika nchi zinazoendelea zikipunguza ukwasi katika fedha zao”
amesema Dkt. Misango.
Amebainisha kuwa Benki Kuu nchini Marekani walipunguza ukwasi kwa kiasi kikubwa na kusababisha riba katika masoko yao kuongezeka, hivyo pesa za mitaji zilizokuwa zinaelekea katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zilipungua.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Januari mpaka sasa nchini Marekani wameanza kupunguza ukwasi, hivyo ni ishara ya kuanza kutoa pesa za mitaji katika nchini zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
“Kadri ya bei ya bidhaa inavyozidi kushuka katika soko la dunia mahitaji ya pesa ya kigeni yanazidi kupungua” amesema Dkt. Misango
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa semina kwa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania kwa ajili ya kueleza namna uchumi wa duniani ulivyoathiri uchumi wa Tanzania na nchi zinazoendelea hasa katika upatikanaji wa fedha za kigeni nchini.