*Asema Mahakama ilishazuia kuwapo kwa muunganiko huo,
*Asisitiza Serikali kupitia Tume ya Ushindani haipaswi kwenda kinyume
Na Mwandishi Wetu
HATIMAYE Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ameamua kuvunja ukimya kwa kueleza kuwa wanasheria waliipotosha Serikali na Mawaziri kuhusu kuendelea na mchakato wa kampuni ya Saruji ya Twiga kununua hisa za Tanga Cement wakati mahakama ilizuia kuwapo kwa muunganiko wa kampuni hizo.
Pia amesema tayari Baraza la Ushindani wa Biashara (FCT) lilishatoa uamuzi wa kuzuia muunganiko wa kampuni hizo baada ya wadau waliopinga suala hilo kufungua shauri na hatimaye kutolewa zuio.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Jaji Mihayo amewaambia waandishi wa habari baada ya kupitia hatua kwa hatua uamuzi wa kisheria uliotolewa, ameshangazwa na hatua ya Serikali ya kuendelea na mchakato ilhali ulishazuiwa.
Jaji Mihayo amesema Mahakama ikishaamua jambo, liwe zuri au baya, linapaswa kuheshimiwa. Kwenda kinyume cha uamuzi wa mahakama ni kuidharau mahakama. Katika suala hili la muunganiko wa Twiga na Tanga Cement mahakama ilishatoa uamuzi kwamba jambo hilo halipaswi kuendelea.
Amesisitiza kwa mantiki hiyo Serikali kupitia FCC (Tume ya Ushindani) haikupaswa kwenda kinyume bali kuheshimu. Kama ilikuwa haijaridhika, kwa mujibu wa FCA (Sheria ya Ushindani), ilipaswa kuiomba FCT kufanya marejeo ya jambo hilo badala ya kuendelea. ” Hi ni kuidharau mahakama.”
Wakati wa majumuishi ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Asharu Kijaji, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi, walisimama bungeni na kutetea uamuzi wa kuendelea na mchakato huo huku wakibainisha kwamba serikali haijavunja sharia.
Dk. Kijaji na Dk. Nchemba walisema serikali iliamua kuendelea na mchakato kwa kuwa mazingira ya awali kwa maana ya soko, yalikuwa yamebadilika na kwamba hakukua na zuio katika mchakato mpya bali ile wa kwanza.
Hata hivyo Jaji Mihayo wakati anatoa mtazamo wake binafsi kama mwanasheria nguli nchini wakati anaelezea hoja za mawaziri hao amesema hata kama mazingira yalikuwa yamebadilika suala hilo lilikuwa limezuiwa bila masharti yoyote, hivyo sheria imekikuwa na amri ya mahakama imedharauliwa.
Amesema kwamba “Kinachoonekana dhahiri hapa kutokana na kauli za mawaziri ni kwamba wanasheria katika wizara husika waliwapotosha mawaziri na serikali kwa ujumla kuhusu suala hili. Mahakama ikishatoa uamuzi na kama hakuna aliyepinga au uamuzi huo kutenguliwa unabaki kuwa sahihi. Kwa hiyo kufanya kinyume cha uamuzi au amri iliyotolewa ni kuidharau mahakama.
” Kuwapo kwa jambo kama hilo, la kutotii uamuzi au amri ya mahakama katika nchi inayofuata utawala wa sheria ni hatari kwa maslahi ya taifa na hata maendeleo kwa ujumla. Ukweli ni kwamba jambo hilo halileti picha nzuri katika utawala wa sheria, “amesema Jaji Mihayo ambaye pia alitumia nafasi hiyo kujibu maswali ya waandishi wa habari waliokuwa wanataka kufahamu vema suala la mchakato huo.
FCC ilitangaza muunganiko wa kampuni kupitia Scancem International DA ambayo ni sehemu ya Heilderberg Cement inayomiliki Twiga Cement na Tanga Cement, jambo ambalo lilipingwa na lilipingwa FCT na wadau wa saruji ambao ni kampuni ya Saruji ya Chalinze, Chama cha Kutetea Haki za Watumiaji wa Bidhaa na Peter Heller kwamba kunaweza kutokea athari katika soko la saruji.
Walisema iwapo Twiga itaruhusiwa kununua hisa za Tanga Cement, kuna uwezekano wa kuwapo na ukiritimba katika soko kwa kuwa Twiga Cement kupitia muungananiko huo, itakuwa na zaidi ya asilimia 68 katika soko. Hali hiyo, walisema inaweza kusababisha upangaji wa bei, hivyo watumiaji wa bidhaa kushindwa kumudu gharama.
FCT ilikubali maombi hayo na kutoa uamuzi kwamba mchakato huo unazuiwa, hivyo hakuna chochote kinachopaswa kuendelea lakini baadaye FCC ilitangaza upya mchakato huo na kuipa Twiga Cement nafasi ya kununua hisa kama mwekezaji ndani ya Tanga Cement.
Kutokana na hatua hiyo, wadau wanaopinga ununuzi huo, waliwasilisha maombi kutaka FCT kukazia hukumu iliyotoa juu ya katazo la kuendelea kwa mchakato huo. Wadau hao walisema kitendo cha FCC kuendelea na mchakato huo ilhali kuna zuio la kufanyika kwa jambo hilo, ni kinyume cha sheria zinazosimamia masuala ya miunganiko ya kampuni kwa kuwa suala hilo lilishasimamishwa.
Wakili Mkuu wa Kampuni ya Mawakili ya MSL Attorneys wanaowatetea wadau hao, Melkisedech Lutema, akizungumza hivi karibuni baada ya kuendelea kwa mchakato huo, alisema kitendo cha FCC kuendelea na mchakato wakati kuna uamuzi wa kisheria kuzuia suala hilo, ni ukiukwaji mkubwa wa kisheria.
“Kisheria, jambo lolote likitolewa uamuzi katika chombo chochote kilichowekwa kisheria, halipaswi kuendelea kufanyika. Na suala la muunganiko wa Twiga na Tanga Cement limezuiwa na hakuna mtu aliyepinga kwa kukata rufani au kuomba mapitio.
“Ni muhimu ikaeleweka kuwa uamuzi uwe sawa au si sawa na hakuna mtu aliyeupinga ni lazima uheshimiweKwa hiyo mtu yeyote anayeendelea anakiuka sheria na anapaswa kuchukuliwa hatua. Kwa hili tumeiomba FCT kukazia hukumu ili uvunjaji huu wa sheria usiendelee,” alisema Lutema.