Na. Sixmund Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii imeshauriwa kuanzisha na kuhamasisha Makumbusho zaidi nchini ili kuhifadhi Urithi wa Kihistoria kwa maslai mapana ya kizazi kilichopo na Kijacho.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhe. Stela Manyanya Leo Bungeni Jijini Dodoma, alipo kuwa akichangia kwenye Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mhe. Manyanya ameongeza kuwa, Makumbusho zilizopo zimeendelea kuipatia heshma nchi kwa uhifadhi na uelimishaji jamii juu ya Urithi wa Kihistoria na Malikale hasa kwa Wageni wakubwa na mashuhuri Duniani wanapozitembelea Makumbusho hizo.
Licha ya kuipongeza Wizara Kwa Makumbusho iliyohifadhi historia adhimu ya Vita vya Majimaji iliyopo Songea Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Manyanya ameishauri Wizara hiyo kuhakikisha inamaliza kiu ya Wananchi wa Nandete Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi, ya kuwa na Makumbusho ya Kihistoria kwenye eneo hilo lililobeba historia kubwa ya Vita vya Majimaji.