NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
MBUNGE
wa Jimbo la Mbagala jijini Dar es Salaam, Mhe. Abdallah Chaurembo amewaambia
wapiga kura wake wa Mbagala Kiburugwa kujiandaa na zoezi la urasimishaji ardhi/majengo
linalotarajiwa kuanza hivi karibuni
kwenye eneo hilo.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na uongozi wa Serikali ya mtaa wa
Kiburugwa kwenye viwanja vya Kwa-Njau, Juni 4, 2023, Mhe. Chaurembo alisema urasimishaji
wa ardhi/majengo ni kutambua miliki za wananchi kwenye maeneo yaliyoendelezwa bila
kupimwa kisheria.
“Wengi
wenu mnamiliki ardhi au nyumba kwa kutumia makaratasi mliyoandikishiana ambayo hayatambuliki
kisheria na baadhi yenu mna leseni za makazi ambazo zilikuwa za kipindi cha
muda fulani na nyingi zimekwisha muda wake na matokeo ya urasimishaji ni kutoa
hatimiliki inayotambulika kisheria.” Alifafanua.
Alisema
zoezi hilo ni shirikishi na kwamba wananchi wakiafiki, wataletwa wataalamu wa
upimaji ardhi na kutoa elimu ya jinsi zoezi hilo litakavyoendeshwa ikiwa ni pamoja na gharama ambazo
mwananchi anapaswa kuchangia ili ardhi/jengo lake liweze kupimwa na kupatiwa
hati miliki ya serikali.
Alisema urasimishaji mbali na kuipa thamani ardhi/nyumba lakini pia utasaidia kuboresha
makazi hususan kwa kuweka miundombinu ya msingi ili kurahisisha usafiri,
kupunguza madhara yatokanayo na majanga mbalimbali kama vile mafuriko na moto.
Zoezi
la urasimishaji lilizinduliwa mwaka 2013 na aliyekuwa waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makzi, Mhe. William Lukuvi na limefanyika maeneo mbalimbali ya
nchi na lengo lilikuwa ifikapo mwaka huu wa 2023 liwe limekamilika.
Awali
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kiburugwa Bw. Abdallah Mpili pamoja na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu mtaa huo ikiwemo masuala ya ulinzi jamii, usafi wa mazingira, ujenzi wa ofisi ya Srrikali ya mtaa, aliwahakikishia wananchi kuwa zoezi hilo litafanyika kwa uwazi na kwa kushirikisha wananchi.
“Wapima
ardhi watakapokuja hapa tutajadiliana nao na kukubaliana jinsi zoezi litakavyoendeshwa ikiwa ni pamoja na gharama ambazo kila mwananchi (mwenye ardhi.nyumba) atapaswa kuchangia.”
Alisema tayari mitaa jirani na mtaa huo wameshafanya zoezi hilo.