Na Mwandishi wetu, Moshi
MAMIA ya wakazi wa Mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara, wakiwemo wadau wa madini na viongozi mbalimbali wamejitokeza kwenye Kijiji cha Kirueni Mwika Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, kumzika Meshack Mwanga, mtoto wa mchimbaji maarufu wa madini nchini Godlisten Mwanga.
Godlisten Mwanga ni Mkurugenzi wa kampuni ya God Mwanga Gems LTD, G & M, GodMwanga & Family investment, Permanut, Mbambabay Coal, GMG Graphite, inayochimba madini mbalimbali nchini ikiwemo Tanzanite, Graphite na makaa ya mawe.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema Godlisten Mwanga ni mwekezaji kwenye eneo lao hivyo wanampa pole na wameshiriki kutoa pole kwenye msiba huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Saitoti Zelothe amempa pole Godlisten Mwanga kwani wamefika kushiriki maziko na kuwapa moyo familia kutokana na kuondokewa na kijana wao.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya kaskazini, Godbless Lema ametoa pole kwa familia ya Godlisten Mwanga kwa msiba huo wa kufiwa na mtoto wao.
Askofu wa kanisa la Pentekoste Sommy Severua amewapa moyo familia kwa kuondokewa na mtoto ambaye amelala na leo June 5 anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.
Akizungumza kwa niaba ya waislamu, usataadh Rajesh William amesema Godlisten Mwanga hana ubaguzi wa dini nao wanamuona kama muislamu mwenzao hivyo wanampa pole.
Henry Mwanga ambaye ni kaka wa marehemu amesema Meshack amezaliwa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, May 17 mwaka 2000 akiwa mtoto wa nne wa Godlisten Mwanga na mama Siah Mwanga.
Amesema Meshack alipata elimu ya msingi Arusha Alliance Primary school ya jijini Arusha mwaka 2007 hadi mwaka 2014 na shule ya sekondari Agape Lutheran Junior Seminary mwaka 2015 hadi mwaka 2018 na chuo cha uhasibu Arusha mwaka 2019 hadi mwaka 2021.
“Mwezi Juni mwaka 2022 Meshack aliajiriwa katika kampuni ya God Mwanga Gems LTD katika nafasi ya dispatch supervisor hadi mauti ilipomkuta,” amesema.
Amesema Meshack alipata ajali ya pikipiki May 4 mwaka 2023 Wilayani Handeni akaumia kichwani na kukimbizwa hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam na kulazwa kwa wiki tatu hadi June mosi alipofariki dunia.