Viongozi wa Jeshi la Polisi wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
……………
Jeshi la Polisi Nchini leo Juni 05, 2023 limepatiwa elimu ya mafao toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kiutendaji baina ya taasisi hizo katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja.
Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Jeshi hilo Naibu Kamishna wa Polisi DCP Gabriel Semiono kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi amesema elimu hiyo itasaidia Askari wa Jeshi hilo kupata uelewa wa pamoja kuhusiana na mabadaliko ya sheria mbalimbali za uendeshaji wa mifuko ya Kijamii.
DCP Semiono amebainisha kuwa kupitia elimu hiyo ambayo wataipata wataenda kutatua kero pamoja na changamoto mbalimbali ambazo Askari wanakumbana nazo wakati wakifuatilia stahiki zao za mafao hususani pindi wanapostaafu kazi.
Aidha amewataka washiriki wote kufuatilia kwa makini mada zote zitakazotolewa lakini pia kutoa maoni na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi.
Kwa upande wake Bwana Mbaruku Magawa ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji katika Mfuko huo amesema lengo la kikao hicho ni kutoa elimu kwa wanachama wake pamoja na kupokea mrejesho wa huduma wanazozitoa kwa jeshi hilo.
Halikadhalika amebainisha kuwa baada ya semina hiyo anaamini kutakua na mabadiliko makubwa katika utendaji wa kazi hususani katika kutoa huduma bora kwa wateja.
Kikao hicho ambacho kinafanyika kwa siku mbili kuanzia Juni 05, 2023 hadi Juni 06, 2023 katika Hoteli ya Gold Crest Jijini Arusha kinahudhuriwa na Maafisa na Askari toka Jeshi la Polisi kitengo cha Mafao na Fidia pamoja na Maafisa toka Mfuko wa Mafao PSSSF.