Na John Walter-Manyara
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imewataka wanafunzi wanaohitimu vyuo vya ufundi katika fani ya umeme kuwa na leseni inayowatambua kulingana na viwango vyao.
Hayo yamesemwa leo Juni 5, 2023 na Meneja wa Ewura Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Lorivii Long’idu wakati akizungumza na wanafunzi wa masomo ya umeme katika Chuo cha Ufundi Veta Manyara kilichopo mjini Babati, wakati wa utoaji elimu maalum kwa wanafunzi hao juu ya umuhimu wa kuwa na leseni.
Amesema leseni hizo zina madaraja tofauti na zinatolewa kwa kuzingatia ujuzi, elimu na uzoefu katika kufunga umeme wenye msongo husika.
Mhandisi huyo amesema kutokana na sera ya serikali ya kupeleka umeme vijiji vyote lakini pia wananchi na taasisis mbalimbali kuendelea kujenga kila siku, kuna uhitaji mkubwa wa mafundi umeme.
Naye Mhandisi Tegemea Kamando, amesema kuwa na leseni ni takwa la kisheria kifungu cha 5(a) cha Sheria ya umeme Sura ya 131, ambacho kinaipa Ewura mamlaka ya kutoa leseni kwa watoa huduma mbalimbali katika sekta ya umeme
Mhandisi Kamando amesema wanatoa leseni kwa waliohitimu mafunzo ya muda mfupi, diploma hadi digrii isipokuwa kwa wafanyakazi wa TANESCO
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa chuo cha VETA Manyara, Msajili wa wanafunzi Sulpisi Awe ameishukuru mamlaka hiyo kwa kuwaelimisha wanafunzi hao na kwamba watakapohitimu wataweza kujiajiri na kuajiriwa bila vikwazo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Israel Sebastian amesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ha kisheria pindi wanapomaliza chuo.