Na mwandishi wetu, Mirerani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, umempongeza Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Mrakibu wa polisi (SP) Dominick Fwaja na askari wake kwa namna wanavyofanya utendaji kazi wao wa kila siku wa kupambana na uhalifu.
Afisa wa TAKUKURU Mji mdogo wa Mirerani, Sultan Ng’aladzi ametoa pongezi hizo kwenye kikao cha TAKUKURU rafiki cha kukutana na kuzungumza na viongozi, makundi mbalimbali na wananchi kwa lengo la kutoa changamoto zilizopo kwenye sekta ya maji, elimu, afya, barabara, ardhi, TANESCO, Polisi na maeneo mengine.
Sultan amesema askari Polisi wa Mirerani wakiongozwa na Mkuu wa kituo hicho SP Dominick Fwaja, wanafanya kazi kubwa hivyo wanastahili kupatiwa pongezi.
Amesema wameona kazi nzuri na kasi kubwa ya polisi kupambana na uhalifu na kukamata dawa za kulevya hivyo jamii iendelee kuwapa ushirikiano wa kutosha.
“Tatizo linakuja pale mtu anapokamatwa akiwa amehisiwa kufanya uhalifu na kufikishwa kituoni au bodaboda wakikamatwa, viongozi na jamii wanatetea hata kabla uchunguzi haujafanyika kwani wanapaswa wawaachie polisi wafanye kazi zao,” amesema Sultan.
Amesema ni wajibu wa polisi kutenda kazi zao bila kuwaonea raia wanaowazunguka zaidi ya kutimiza wajibu wao wa kila siku kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi amesema utendaji kazi wa polisi wa kituo cha Mirerani wakiongozwa na Mkuu wao SP Fwaja ni wakupongeza.
“Mimi kwa nafasi yangu nikiwa Diwani sijawahi kupata malalamiko ya raia kuonewa na polisi, binafsi na mimi niwapongeze kwa utendaji kazi wao mzuri,” amesema Salome.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliohudhuria kikao hicho wameeleza kuwa askari hao hawapaswi kubweteka zaidi ya kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na weledi.