Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana Juni 2, 2023 amewasili katika Ubalozi wa Tanzania ulioko Jijini Algiers nchini Algeria na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu ikiwa ni maandalizi ya kushuhudia mchezo wa Fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Dar es Salaam Young Africa (Yanga) na USM Alger ya nchini humo utakaochezwa Juni 3, 2023 majira ya saa 2: 00 usiku ambazo ni saa za nchi hiyo, katika Uwanja wa Julai 5, 1962.
Mara baada ya kuwasili katika Ubalozi huo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesaini Kitabu cha Wageni pamoja na kuzungumza na Balozi wa Tanzania nchini humo pamoja na kupata nafasi ya kuzungumza na wachezaji wa Timu ya Yanga katika Kambi yao, ambapo mbali na kuwatakia heri, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. ameahidi zawadi zaidi endapo watabeba Kombe na Watanzania wanawaombea na kuwatakia heri pia.
Katika ziara hiyo Mhe. Chana ameambata na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Tabia Maulid, Mwenyekiti UWT Taifa Mhe. Mary Chatanda, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Ndg. Nicholas Mkapa, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Ndg. Wallace Karia, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na mashabiki.