Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa Elimu kilicholenga kupitia rasimu ya ufafanuzi wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016. Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku tatu, Mei 31 – Juni 2, 2023 mjini Mpanda.
Washiriki wa kikao kazi cha kupitia rasimu ya ufafanuzi wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016, wakimsikiliza Katibu wa TSC wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kinafanyika kwa siku tatu, Mei 31 – Juni 2, 2023 mjini Mpanda.
Mkurugenzi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, Mwl. Fatuma Muya akitoa neno la kumkaribisha Katibu wa TSC ili afungue kikao kazi cha kupitia rasimu ya ufafanuzi wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016. Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku tatu, Mei 31 – Juni 2, 2023 mjini Mpanda.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Katavi anayeshughulikia elimu, Mwl. Pendo Rweyemamu akitoa neno wakati wa kikao kazi cha kupitia rasimu ya ufafanuzi wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016. Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku tatu, Mei 31 – Juni 2, 2023 mjini Mpanda.
Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Mpanda Benson Ng’amilo akitoa neno la ukaribisho wakati wa kikao kazi cha kupitia rasimu ya ufafanuzi wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016. Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku tatu, Mei 31 – Juni 2, 2023 mjini Mpanda.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha wadau wa Elimu cha kupitia rasimu ya ufafanuzi wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016. Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku tatu, Mei 31 – Juni 2, 2023 mjini Mpanda.
W ashiriki wa kikao kazi cha kupitia rasimu ya ufafanuzi wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016, wakiwa katika kazi za vikundi kwa ajili ya kupitia rasimu hiyo. Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku tatu, Mei 31 – Juni 2, 2023 mjini Mpanda.
………………………………
Na Mwandishi wetu – Mpanda, Katavi
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama amesema TSC inaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa walimu katika kuielewa kwa kina Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016 ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mwl. Nkwama ameyasema hayo Mei 31, 2023 mjini Mpanda mkoani Katavi wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu kinachohusisha wadau wa elimu wakiwemo Afisa Elimu wa Mkoa wa Mpanda, Watumishi wa TSC Wilaya ya Mpanda na Makao Makuu Dodoma, Maafisa Elimu, Wathibiti Ubora wa Shule, Chama cha Walimu (CWT) na Walimu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda
Washiriki wa kikao kazi hicho kilichoandaliwa kwa ufadhili wa Mradi wa Shule Bora wana jukumu la kupitia na kufanya maboresho ya rasimu ya Ufafanuzi wa Sheria hiyo kwa lengo la kuiweka katika lugha na tafsiri rahisi itakayoweza kueleweka kwa walimu wote nchini.
Katibu alieleza kuwa walimu wanamekuwa wakifanya kazi kwa bidii jambo ambalo limefanya ufaulu wa wanafunzi kuongezeka, hata hivyo aliweka wazi kuwa wapo walimu wengi ambao hawana uelewa wa kutosha juu ya Sheria na Kanuni hizo zinazosimamia utumishi wao.
“Mwalimu akitulia na kila kitu chake kikitulia kazi yake itakuwa kufundisha watoto tu. Walimu wetu wanafanya kazi vizuri lakini tumebaini kuwa wanachangamoto nyingi ikiwemo kutokuifahamu vizuri Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu ambayo ndiyo inayosimamia utumishi wao. Tunahitaji mwalimu afahamu kila kitu kinachohusu utumishi wake, hivyo kazi hii ikikamilika itakuwa ni mwarobaini wa utatuzi wa changamoto hiyo,” alisema.
Alisema Sheria hiyo pamoja na kanuni zake zimeweka wazi masuala yote yanayohusu namna ya kushughulikia masuala ya Nidhamu, Ajira na Maendeleo ya walimu na pia imeweka vyombo mbalimbali vya kushughulikia masuala hayo.
“Walimu wameheshimishwa sana katika utumishi wao, kwa mfano TSC ngazi ya Wilaya inaundwa na Kamati ya Tume yenye Mwenyekiti, Katibu pamoja na wajumbe wanne (4). Wajumbe hao ni Katibu Tawala Wilaya, Afisa Elimu Wilaya na Walimu wawili (2), mmoja kutoka shule za Msingi na mwingine kutoka Sekondari. Hawa ndio wanaoamua masuala ya Nidhamu na Maendeleo ya Walimu,” alisema.
Aliongeza kuwa mwalimu asiporidhika na uamuzi unaofanywa na TSC Wilaya Sheria imempa fursa ya kukata rufaa Tume Makao Makuu ambayo inaundwa na Mwenyekiti, Katibu pamoja na wajumbe nane kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, na endapo hataridhishwa na uamuzi wa TSC Makao Makuu ana haki ya kukata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katika eneo la ajira na maendeleo ya walimu napo kuna changamoto za walimu kutofahamu taratibu. Kwa mfano, hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kupandisha madaraja watumishi wa Umma wakiwemo walimu, lakini tunapokea simu za malalamiko kutoka kwa walimu wakidai hawajapandishwa lakini wengi wao bado hawajakidhi vigezo kulingana na miongozo iliyopo. Hivyo, unaweza kuona kuwa bado tuna kazi kubwa ya kuwaelimisha walimu wetu,” alisema.
Pamoja na hayo, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali anazofanya katika kuboresha sekta ya elimu ikiwemo kutafuta wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya elimu, kuanzisha mchakato wa kuandaa Sera na Mtaala mpya wa elimu na kueleza kuwa TSC itahakikisha fedha zote zilizoelekezwa katika Tume hiyo zitatumika kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
“Ninaomba kutumia fursa hii kumhakikishia Mhe. Rais wetu kwamba Tume ya Utumishi wa Walimu tunaithamini kazi kubwa anayoifanya. Tunamwahidi kuwa tutahakikisha thamani ya fedha kwa kazi inayofanyika inapatikana na inaonekana ili malengo ya kuboresha elimu nchini yaweze kufikiwa,” alisema.
Akitoa neno la utangulizi, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Katavi anayeshughulikia elimu, Mwl. Pendo Rweyemamu alisema TSC imeendelea kupiga hatua katika kusimamia walimu jambo ambalo limesaidia kuleta utulivu na kufanya walimu kuendelea kutoa huduma kwa walimu.
Vilevile, Mwl. Rweyemamu alishukuru Mradi wa Shule Bora kwa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu katika Mkoa wa Katavi huku akisema Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha mipango yote inakamalika bila vikwazo.
“Tunawashukuru wadau wetu wa Shule Bora kwa kuiwezesha Tume kushiriki kwa karibu na kuhakikisha Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 inafafanuliwa ili iweze kutumika na kueleweka kwa urahisi kwa walimu wetu na wadau wengine. Tunatambua kuwa mmekuwa na miradi mbalimbali ya elimu ndani ya mkoa wetu, jambo hili linaifanya Katavi kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta ya elimu,” alisema.
Mradi wa Shule Bora unafanya kazi katika mikoa tisa Tanzania Bara ambayo ni Rukwa, Katavi, Kigoma, Tanga, Pwani Mara Simiyu, Singida na Dodoma.