Wanahisa wa Benki ya NMB wameidhinisha gawio la Shilingi Bilioni 143.1 kwa mwaka 2022, sawa na shilingi 286 kwa kila hisa moja katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 23 wa Wanahisa uliofanyika kwa njia ya mtandao leo. Hili ni ongezeko la 48% ukilinganisha na gawio la jumla la Shilingi Bilioni 96.7 lililolipwa mwaka 2021.
Benki hiyo ikiwa inaandika historia ya kutimiza miaka 25 ya kuwahudumia watanzania, hili ni gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa na taasisi ya fedha nchini kwa wanahisa wake. Gawio hilo litalipwa kufikia tarehe 14 Juni 2023.
“Miaka minne iliyopita, tulilipa gawio la shilingi bilioni 33 kwa wanahisa wetu, lakini kwa mwaka 2022 gawio limeongezeka na kufikia Shilingi Bilioni 143.1. Ongezeko hili la gawio linaendana na ongezeko la mchango wetu katika uchumi wa taifa letu na maendeleo ya wananchi kupitia programu yetu ya uwajibikaji kwa jamii, ambapo kwa mwaka huu tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 6.2 zinazoelekezwa kwenye sekta ya afya, elimu, mazingira, elimu ya fedha na usaidizi wa majanga,” amesema Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna.
“Mafanikio ya Benki yetu ni matokeo ya mazingira mazuri ya kibiashara yaliowekwa na Serikali yetu, Imani ya wanahisa na wateja wetu, juhudi za wafanyakazi wetu, usimamizi mzuri wa Benki Kuu ya Tanzania na ushirikiano mzuri uliopo na wadau wetu wote. Tunawashukuru na tuendelee kuwa pamoja katika safari yetu ya mafanikio,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt. Edwin P. Mhede amesema: “Bodi yetu itaendelea kuwa ya kibunifu na kusimamia ukuaji wa Benki ili kuhakikisha wanahisa wetu wanaendelea kunufaika na uwekezaji wao. Bodi ina imani kubwa na mikakati iliyopo na imedhamiria kuhakikisha NMB inaendelea kuwa Benki kiongozi nchini na inakuwa na mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii.”