……
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Madini, Dkt. Dotto Biteko afuatilie taasisi za fedha zinazowakopesha wachimbaji wadogo kwa kuangalia viwango vya riba vinavyotolewa na aina ya shughuli wanazozifanya wajasiriamali hao ili kurahisisha urejeshwaji wa mikopo.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni Mosi, 2023) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mazingira rafiki ya upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo kulingana na uhalisia wa biashara zao.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua changamoto ya masharti mbalimbali kwa taasisi za kifedha, hivyo imetoa maelekezo kwa taasisi hizo kuwa zitambue aina ya shughuli zinazofanywa na wajasiriamali hao na muda unaotumika kuanzia uwekezaji hadi uzalishaji wake ili masharti yaendane na shughuli husika.
Pia, Waziri Mkuu amewashauri wajasiriamali hao wajiunge katika vikundi ili waweze kupata mikopo inayotolewa na Serikali (asilimia 10 ya mapato ya halmashari), mifuko ya uwezeshaji pamoja na inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wote katika maeneo yanayonufaika na fedha za uwajibikaji (CSR) kutokana na miradi mbalimbali ya uwekezaji wahakikishe wanazisimamia vizuri na kuzitambulisha kwenye Mabaraza ya Madiwani ili waweze kuzipangia utaratibu matumizi kama ilivyokusudiwa.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Busega, Simon Songe aliyetaka kujua ni nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha fedha za CSR zinatumika kwa wakati pindi zinapofikishwa katika maeneo husika.
Amesema fedha hizo za CSR zinapaswa kuingia kwenye mfuko wa mapato ya ndani ya kijiji au halmashauri ili iweze kuratibiwa na kupangiwa miradi ya kutekeleza kulingana na mahitaji ya jamii husika. “Fedha hii inapoingia inakuwa sehemu ya bajeti na ni lazima itumike na Serikali inazisimamia kupitia halmashauri zetu.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa vibali kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kuajiri watumishi wa sekta ya afya ili waweze kwenda kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yote ya kutolea huduma hizo zikiwemo zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Amesema hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa ujenzi wa maeneo ya kutolea huduma za afya nchini zikiwemo zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri za wilaya, mikoa na kanda. “Kazi nyingine inayoendelea kwa kasi ni ya kupeleka vifaa tiba na dawa.”
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliyetaka kufahamu ni upi mpango wa Serikali katika kuhakikisha miundombinu iliyopo katika maeneo ya kutolea huduma za afya na vifaa vinaendana na utoaji huduma wa uhakika kwa kupitia uwepo wa wataalamu wa kutosha.
“Kazi kubwa imefanywa nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake na kwa usimamizi wake, sisi tutaendelea kuimarisha maeneo hayo ya utoaji huduma na Serikali itaendelea kujenga miundombinu hiyo kulingana na mahitaji ya eneo husika.”
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa ametaja mpango mwingine wa Serikali katika kukabiliana na changamoto ua upungufu wa watumishi kuwa ni pamoja na kufanya mapitio ya ikama ya watumishi na kwa kuhamisha watumishi katika maeneo yenye watumishi wengi na kuwapeleka kwenye upungufu.
IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU, ALHAMISI, JUNI MOSI, 2023.