Na Farida Mangube Morogoro.
Serikali imeahidi kuendelea kutatua changamoto zinazowakabli vijana kote nchi ili waweze kuendelea kushiriki shughuli za kiuchumi kwa lengo la kukuza pato lao na pato la Taifa.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima, wakati alipokuwa akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Kumbukizi ya 18 ya Waziri Mkuu wa zamani Hayati Edward Moringe Sokoine, iliyofanyika katika viunga vya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, mjini Morogoro.
Mhe. Nguli amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imekuwa ikipambana na changamoto zinazowakabili vijana na kuwekeza nguvu kubwa katika maeneo ambayo vijana watafaidika kiuchumi.
“ Kwa sasa kuna Mpango wa Mageuzi ya Kilimo (BBT), ambapo serikali imejipanga kisawasawa kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki katika kilimo chenye tija kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri katika sekta hiyo muhimu.” Alisema Nguli.
Ameongeza kusema kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 takwimu zinaonesha kuwa kundi kubwa la Watanzania ni vijana hivyo serikali imeweka mikakati kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki shughuli za uchumi kwa kuwawezesha kujiajiri katika sekta mbali mbali.
“Ninawapongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuja na kauli mbiu nzuri ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema kuwa “Mazingira Wezeshi kwa Vijana Kushiriki Katika kilimo Tanzania: Sera, Miongozo na na Utendaji” ni kauli mbiu muafaka kwani ndicho serikali inachokifanya kwa sasa kuwezesha kundi la vijana kuzalisha mazao ya kilimo na mnyororo wa thamani, sambamba na shughuli nyingine za uzalishaji”.Alisema
Nguli akiwataka vijana kote nchini kuacha kubweteka kwa kuendekeza starehe na kujikita katika kufanya kazi ili waweze kuepukana na utegemezi.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo ya kumbukizi ya 18 ya Hayati Sokoine, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Jaji Joseph Sinde Warioba, Alisema SUA itaendelea kuwa kitovu cha kuwajenga vijana Katika Kilimo.