SERIKALI inatarajia kupokea ndege ya kwanza ya mizigo aina ya Boeing 767 -300Fmnamo tarehe Tatu Juni itakayokwenda kutatua changamoto za usafirishaji wa mizigo kwa wafanyabiashara nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Juni 1,2023 Jijini Dar es Salaam, Waziri Wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kukosekana kwa ndege ya mizigo toka nchini kwenda nchi za nje kumechangia ucheleweshwaji wa bidhaa pamoja na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji.
“Zaidi ya Tani elfu 24 za bidhaa ya samaki, mbogamboga na maua toka nchini zimekuwa zikisafirishwa kupitia viwanja vya ndege vya nje ya Tanzania lakini ujio wa ndege hii utatoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo kusafirisha mizigo kwa gharama nafuu na kwa urahisi”, amesema Prof.Mbarawa
Aidha amesema tukio hilo la kupokea ndege litafanyika katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi katika tukio hilo anatarajiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mbarawa ameongeza kuwa Serikali iliamua kununua ndege hiyo kwa kuzingatia unafuu wake wa matumizi ya mafuta na kusema ndege hiyo itakuwa na uwezo wa kufanya safari kwa saa kumi bila kutua kiwanja chochote.
Naye Afisa uhusiano wa Shirika la Ndege Tanzania Bi.Sarah Ruben amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji nchini kuwa ndege hiyo itakuwa na ratiba maalum itakayotoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuweza kuitumia.