Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na Wadau wa Barabara (hawapo pichan) wakati alipofungua Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Barabara Duniani unaofanyika jijini Arusha.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Barabarabaada ya kufungua Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Barabara Duniani unaofanyika jijini Arusha.
…….
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amewataka watalaam wa barabara kutafuta suluhisho na mwarobaini wa changamoto zinazoikabilia miundombinu ya barabara mijini ikiwemo kupunguza msongamano wa magari na uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya miji.
Amesema hayo Jijini Arusha katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC), wakati akifungua kongamano la Kimataifa la Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC) litakalofanyika kwa siku tatu na kuhusisha wataalam wa hapa nchini, nchi za Afrika, Ulaya na Asia.
“Barabara ni mhimili mkubwa kwa nchi yetu kwani mizigo mingi inayotoka na inayoingia nchini kupitia Bandari husafirishwa barabarani ” ameeleza Prof. Mbarawa.Prof.
Mbarawa ameeleza kuwa pamoja na kuboresha njia nyingine za usafiri kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa reli ya kati na ujenzi wa reli ya kisasa kwa ajili ya kuipunguzia mzigo mkubwa barabara katika usafirishaji wa mizigo hasa inayokwenda mikoa ya mbali na bandari na nje ya nchi.
Aidha amewaagiza watalaam kukamilisha taarifa sahihi za kisayansi na kuwasilisha Wizarani wakati Serikali ikijiiandaa kufanya marekebisho ya Sera ya barabara hususani kwenye eneo la matumizi sahihi ya matairi mapana ‘Super Single’ hapa nchini ikiwa ni lengo la kuzilinda barabara nchini.
“Katika Mkutano huu mmejaa wabobezi kwenye mambo ya barabara ninachotegemea baada ya kikao hiki pamoja na mambo mengine mniletee utafiti uliofanywa kuhusu matumizi sahihi ya matairi mapana (super single tyre) ili tuweze kufanya maamuzi sahihi kwa Taifa letu” ameongeza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TARA, Bw, Joseph Haule ameeleza kuwa semina hiyo ya Kimataifa inayohusu masuala ya usafirishaji endelevu wa mizigo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii imendaliwa na Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC) kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) na Chama cha Wadau wa BarabaraTanzania (TARA) lengo likiwa ni kujadili na kutafuta ufumbuzi masuala mbalimbali ya barabara na hivyo kuleta tija.