Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Timu ya Watafiti na Wataalamu wabobevu wa masuala ya lishe nchini wakiongoza na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wakutana kwenye mafunzo ya siku nne kuwajengea uwezo kabla ya kuanza zoezi la Kitaifa la kufaya tathimini ya haraka ya visababishi na viashiria vya utapiamlo na udumavu katika mikoa nane ya Tanzania.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Mwita Waibe amesema kazi hiyo waliyopewa kikosi kazi hicho cha kitaifa ni matokeo ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka kupunguza na kumaliza kabisa tatizo la utapiamlo na udumavu nchini kupitia utafiti wa kina na majibu atakayokabidhiwa na kikosi kazi hicho.“Katika Mjadala wa Marais ambao una Marais zaidi ya kumi wa Afrika Rais wetu amepewa jukumu la kuwa kiongozi wa timu hiyo katika kusimamia tatizo la utapiamlo na udumavu katika nchi masikini, kwa muktadha huo wakiwa Marekani kwenye mkutano wao ndipo alipopata nafasi ya kuongea na ‘Big win Philanthropy’ ambao walikubali kutoa msaada wa kumsaidia Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza kazi hii ambayo kikosi kazi hiki kimeanza kuifanya ili kuja na majibu ya kisayansi ambayo atayafanyia kazi”, ameeleza Bwana Waibe.
Mkurugenzi huyo amesema takwimu za ‘demographic’ za mwaka jana zilizoonesha Tanzana ina udumavu kwa asilimia 30 na takwimu hizo ndizo zilizoifanya nchi kupata msaada huo kwa haraka maana nchi ya aina hiyo haiwezi kuendelea kama ina watu asilimia 30 ambao hawawezi kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.
Ameongeza kuwa changamoto hiyo ndiyo iliyomsukuma Mhe. Rais kutaka kupata majibu sahihi ya kisayansi ya visababishi na viashiria vya tatizo hilo nchini ikizingatiwa kuwa mkoa kama Iringa ambao una vyakula vya kila aina na hali nzuri ya hewa lakini inaongoza kuwa na udumavu kwa asilimia zaidi ya 50.
“Tatizo hilo sio tuu kwa Iringa lakini mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini na Mhe. Rais akajiuliza pamoja na mikataba aliyosaini na wakuu wa mikoa na rasiliamali anazozitoa katika kupambana na tatizo hili lakini bado haliishi hivyo akaona kuna sababu za kupata timu ya Watanzania wabobevu ambao watampatia majibu sahihi ili yaweze kumsaidia kujua ni nini hasa kifanyike ili kumaliza tatizo hilo nchini pale Benki ya Maendeleo ya Afrika na wadau wengine aliozungumza nao watakapompatia fedha, ndipo akamua itangazwe tenda watalamu na taasisi mbalimbali ziombe kuifanya lakini SUA wakashinda kuifanya kazi hiyo ya Mhe. Rais na anayasubiria majibu kwa hamu sana”, ameeleza Bwana Waibe.
Amewapongeza SUA kwa kushinda kufanya kazi hiyo kubwa ya nchi na kuwashukuru kwa kukubali ombi la serikali la kushirikiana na taasisi zingine kwenye kufanya kazi hiyo akiamini kuwa watakuja na mpango na majibu sahihi ambayo nchi itayatumia katika kutatua changamoto ya utapiamlo na udumavu nchini.
Kwa upande wake Mtafiti Kiongozi wa kikosi kazi hicho kutoka Idara ya Sayansi za Chakula na Studi za Walaji (SUA) Prof. John Msuya amesema utafiti huo utafanyika katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Mtwara, Geita, Njombe, Dar es Salaam, Tabora na Iringa na mikoa miwili ya Tanzania Zanzibar ambayo ni Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.
Amesema uchaguzi wa mikoa hiyo umezingatia mabadiliko makubwa ya tatizo hilo yaliyoonekana kwenye taarifa za mwaka 2015 na 2022 ambapo kuna mikoa imefanikiwa kupunguza tatizo katika kipindi hicho na mingine hali imeongezeka hivyo kuna kitu cha kujifunza kwa mikoa iliyofanikiwa na ile iliyoshuka.
“Ukiangalia taarifa za mwaka 2015 Mkoa wa Mtwara ulikuwa na udumavu kwa asilimia 38 lakini mwaka 2022 wamepunguza na kufikia asilimia 22, Kaskazini Pembe kutoka asilimia 34 mwaka 2015 hadi 21 mwka 2022 lakini na ukiangalia Dar es Salaam imepanda udumavu kutoka asilimia 15 mwaka 2015 hadi asilimia 18.40 mwaka 2022, Iringa kutoka asilimia 42 mwaka 2015 hadi asilimia 56.90 mwaka 2022 huku kwa upande wa Zanzibar Kaskazini Unguja ikipanda kutoka asilimia 23 mwaka 2015 hadi asilimia 29 mwaka 2022”,amefafanua Prof. Msuya.
Amesema timu hiyo ya watafiti inakwenda kuangalia mambo makuu mawili ambayo nikutafiti kama matunzo ya watoto yanaweza kuwa kisababishi cha utapiamlo na udumavu katika mikoa iliyochaguliwa lakini jambo lingine kubwa ni kutambua na kuchambua mifumo na tabia sababishi za utapiamlo na udumavu kwenye mikoa hiyo.
Akitoa salamu za Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Fedha na Mipango Prof. Amandus Muharwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha washirki wote wa zoezi hilo kuwa na mbinu bora na sahihi za ukusanyaji wa taarifa za kitafiti ili kufikia kusudio la serikali la kuainisha visababishi vya lishe duni nchini na hatimae kutumia ufahamu huo katika kutengeneza mipango na mikakati ya kutokomeza tatizo hilo.
“Mafunzo haya ni muendelezo wa dhamira njema ya serikali ya kuboresha hali ya lishe chini na kupunguza udumavu kwa watoto wetu walio chini ya umri wa miaka mitano hali ambayo inarudisha nyuma afya na maendeleo ya watu wetu”, amesema Prof. Mhairwa.
Naibu huyo wa Makamu Mkuu wa Chuo Utawala Fedha na Mipango ametumia nafasi hiyo kuihakikishia serikali kama wasimamizi wakuu wa utafiti huo kuifanya kazi hiyo maalumu ya Kitaifa ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa weledi na ubora unaotakiwa ili taifa liweze kuondokana na tatizo hilo kubwa kwa wananchi wake.
Kikosi Kazi hicho kinajumlisha wataalamu watano kutoka SUA, mmoja kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara, maafisa nane waandamizi kutoka Wizara ya Afya, Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Taasisi ya lishe na Chakula, washiriki wengine nane kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa wakishirikina na wataalamu na maafisa wa serikali na Ofisi ya Rais TAMISEMI.