Na Mwandishi Wetu
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akishiriki filamu ya Royal Tour, moja ya lengo lake ilikuwa pia kuonesha madhara ya ujangili kwa maliasili za Tanzania.
Ndio maana katikati mwa filamu ya Royal Tour Rais anaonekana akiwa na Mwongozaji wa Filamu hiyo wakiwa sehemu ya maghala ya meno na pembe za ndovu.
Kwa masikitiko katika Royal Tour Rais Samia anasikika akisema: “Nyara hizi hatuwezi kuziuza wala kuziteketeza, zitaendelea kubaki hapa milele kama ushahidi kwa vizazi vijavyo kuwa ukatili kwa wanyama haufai.”
Leo Mei 31, watendaji waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni kama “wamemfuta machozi” Mhe Rais kwa kuzindua mkakati wa kitaifa wa kutokomeza ujangili.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika leo jijini Dodoma, Waziri wa sekta hizo Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa onyo kali kwa majangili katika wakati huu ambapo vitendo hivyo vimepungua sana.
“Vitendo vimepungua na maliasili zetu zimepumua lakini tutaendelea kujiimarisha na natoa onyo kali kwa wanaojaribu kuendelea na biashara hii haramu ni bora wabuni shughuli nyingine halali za kiuchumi.” Alisema Mhe. Mchengerwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi alitumia sanaa ya ushauri kueleza madhara ya ujangili akighani shairi lisemalo: “Jangili Si Jasiri Bali ni Mtu Dhalili.”