Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena l. Tax amesema kuwa mwezi Novemba 2022, Wizara yake iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 22 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi zilizo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi (IORA) uliofanyika jijini Dhaka, Bangladesh. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya IORA.
Hayo ameyasema leo Mei 30, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.
Dkt. Tax alisema kuwa pamoja na mambo mengine, mkutano huo uliridhia Tanzania kuwa mwenyeji wa Mdahalo wa Tisa wa IORA uliofanyika mwezi Mei 2023 huko Zanzibar.
“Kufanyika kwa mdahalo huo hapa nchini kumetoa fursa kwa wataalam kubadilishana uzoefu, kutangaza utalii na fursa nyingine za uwekezaji, hususan katika uchumi wa buluu”. Alisema Dkt. Tax.
Aidha, mdahalo huo unatajwa kuwa na tija kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa umeimarisha mahusiano ya kikanda baina ya Tanzania na Nchi Wanachama wa IORA.
Fauka ya hayo, katika mkutano wa 22 Tanzania ilifanikiwa kuzishawishi Nchi Wanachama wa IORA kuanzisha utaratibu wa kufanya ukaguzi wa hesabu za Jumuiya hiyo kwa mzunguko (rotational basis). Ambapo kukubalika kwa pendekezo hilo kutaongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za IORA ikilinganishwa na utaratibu wa sasa ambapo ukaguzi unafanywa na nchi ya Mauritius pekee yalipo Makao Makuu.
Aidha, utaratibu huo utatoa fursa kwa wakaguzi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuimarisha uwezo wa kufanya kaguzi katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.