Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Ulinzi wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujadili hali ya Usalama katika Eneo la Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umefanyika jijini Bujumbura, Burundi hivi karibuni.
Akifungua Mkutano
huo, Waziri
wa Ulinzi wa Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Mhe. Alain Tribert Mutabaze, amesema jitihada za pamoja
ikiwemo mikakati mipya ya namna ya kukabiliana na vikundi vya waasi katika eneo
la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado zinahitajika ili
kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika eneo hilo.
Amesema pamoja na kupongeza jitihada nyingi zinazofanywa
na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo kupeleka Kikosi cha Kulinda amani cha
Jumuiya (EACRF), bado ipo haja ya
kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mikakati iliyopo kama inaleta tija na kuandaa
mikakati mipya ikiwa ni pamoja na kuviwezesha
Vikosi hivyo ili viweze kutekeleza kikamilifu
jukumu la kulinda amani katika eneo hilo.
“Changamoto katika eneo la
Mashariki mwa Congo bado zipo. Tunatakiwa kuboresha mikakati yetu na kufanya
tathmini za mara kwa mara ya maendeleo ya jitihada hizi, kwani hali inayoendelea Mashariki mwa Congo
inatuathiri sote kama jumuiya kwa namna moja au nyingine. Hivyo niwaombe
Waheshimiwa Mawaziri tuje na mapendekezo yenye tija tutakayoyawasilisha kwa Wakuu wetu wa Nchi
kwa mustakabali wa eneo hilo la
Mashariki mwa Congo na sisi sote” amesema Mhe. Mutabaze.
Mhe. Mutabaze pia alitumia
fursa hiyo kuwakaribisha Mawaziri hao nchini Burundi na kuwaomba kutumia muda
wao kujadili na kuandaa mapendekezo yatakayoleta suluhu ya kudumu nchini DRC
hususan eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.
Awali akizungumza kwenye
mkutano huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki
amesema Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Nchi Wanachama ili
kuhakikisha amani na utulivu wa kudumu unapatikana katika eneo la Mashariki mwa
Congo.
Mkutano huo umewahusisha
Mawaziri wa Ulinzi kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Makatibu
Wakuu na Wakuu wa Majeshi.
Ujumbe wa Tanzania kwenye
Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe.
Innocent Bashungwa (Mb.) na kumshirikisha pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji
Mnyepe, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko, Mkurugenzi wa
Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Stephen Mbundi pamoja na Maafisa wengine waandamizi kutoka
Serikalini.