Na. Dennis Gondwe, MNADANI
WANANCHI wa Kata ya Mnadani wametakiwa kutokomeza ukatili wa kijinsia ili kuunga mkono juhudi za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kupambana na ukatili huo na kuwaletea maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Viti maalum Jiji la Dodoma, Asma Karim alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Mnadani iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Karim alisema kuwa jukumu la kupinga aina zote za ukatili wa kijinsia ni la jamii nzima. “Ndugu zangu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan hawezi kuja kuingia katika nyumba zetu na kutokomeza ukatili wa kijinsia. Sisi ndiyo jukumu letu kufanya hivyo na kuhakikisha kwamba ukatili wa kijinsia unaisha katika jamii yetu. Wanawake ni wahanga wa ukatili wa kijinsia kutokana na hali za kiuchumi. Umefika wakati kina mama kujikwamua kiuchumi ikiwa ni moja ya mkakati wa kukabiliana na tatizo la ukatili wa kijinsia” alisema Karim.
Aliwataka wananwake kuwa mstari wa mbele katika kulijenga taifa. “Wanawake asili yetu ni uchapa kazi. Tunamuona rais wetu alivyo mchapa kazi, sisi tumuunge mkono kwa kufanya kazi na kuijenga nchi yetu. “Tukizembea na kumtegemea Mheshimiwa Rais pekee haiwezekani, tukimuachia mbunge pekee haiwezekani, tukiwaachia madiwani pekee haiwezekani. Sote kwa umoja wetu lazima tufanye kazi kwa pamoja ili kukuza uchumi wetu” alisema Karim.
Wakati huohuo, aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika malezi ya watoto. “Kina mama nendeni mkalee watoto wetu. Malezi bora ya watoto na uangalizi wa karibu ni msingi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. Malezi bora kwa watoto yatatuwezesha pia kupiga hatua ya maendeleo katika jamii kwa sababu juhudi zenu za uchumi hazitatoa matunda. Mtajenga nyumba, mtatajirika na ninyi mtakuwa zii kwa sababu hakuna kinachoendelea kutokana na kuharibika kutokana na ukatili wa kijinsia” alisema Karim.
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Kata ya Mnadani, Farida Mbarouk aliipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Kata ya Mnadani. “Serikali imefanya mambo makubwa sana kutujengea shule, vituo vya afya na mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba inayotolewa na halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM. Serikali imetujengea madarasa tisa na sasa shule mpya inajengwa. Utekelezaji huu utaongeza ufaulu kwa wanafunzi katika Kata ya Mnadani kwa sababu walimu wapo wa kutosha” alisema Mbarouk.
Alisema kuwa suala la ardhi lilikuwa changamoto kubwa. “Sasa ardhi inapimwa na watu wanamilikishwa viwanja. Suala la miundombinu ipo vizuri, barabara zinapitika muda wote. Maji yanapatikana kila siku” alisema Mbarouk.
Madiwani 14 wa Viti maalum wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanafanya ziara katika kata 41 za jiji hilo kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii na fursa za kiuchumi.