Na. Brigitha Kimario- Serengeti
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaka Menejimeti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kushirikiana na wananchi kutatua migogoro baina ya Hifadhi na wananchi wa maeneo yanayozunguka hifadhi hizo.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Karakatonga kata ya Kwihancha na kijiji cha Kegonga kata ya Nyanungu Wilaya ya Tarime amewataka TANAPA kuelekeza miradi ya ujirani mwema kwenye vijiji hivyo na kutatua migogoro ya mipaka kwa kuwashirikisha wananchi.
“Viongozi wa Hifadhi kaeni na wananchi kupitia ujirani mwema nataka kuona amani, rekebisheni mahusiano yenu”
Aidha, Waziri Mchengerwa amewataka wananchi hao kuwa wazalendo na kuwa chanzo cha kutoa taarifa pale ambapo kuna dalili ya matukio ya ajabu hifadhini.
Mchengerwa amewasisitiza wananchi kufuata sheria za nchi, sheria za mipaka pamoja na sheria za Uhifadhi ili kuepuka migogoro inayojitokeza.
Pia, Waziri Mchengerwa amewaasa viongozi wa chama kutokukata tamaa na kuwaasa waiamini Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni
Serikali sikivu,na inayojali wananchi wake.
Mhe. Mchengerwa ameahidi kuzichukua kero zote na kuzifanyia kazi kwa wakati
na kuahidi kutoa mrejesho kwa wakati.