Na Kassim Nyaki, NCAA
Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga wamefanya ziara katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kujifunza shughuli za Uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii na kueleza kuwa wapo tayari kuwapokea wananchi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari.
Hatua hiyo inakuja kufuatia mpango wa Serikali kuanza ujenzi wa nyumba 5,000 katika eneo la Kitwai Wilayani Kilindi Mkoani Tanga kwa ajili kuhamisha wananchi waliojiandikisha kuhama kwa hiari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Mhe. Idrisa Omari Mgaza aliyeongoza ujumbe wa Madiwani hao ameeleza kuwa uongozi wa Wilaya hiyo unaunga mkono uamuzi wa wananchi wa Ngorongoro wanajiandikisha kuhama kwa hiari.
“Serikali imetushirikisha kuhusu mradi wa uhamishaji wa wananchi wa Ngorongoro kuja Wilaya ya Kilindi, sisi kama viongozi tutatoa ushirikiano na kuhakikisha nyumba 5,000 zinajengwa katika kata ya Saunyi na maeneo mengine, Nyumba zikikamilika wananchi waliojiandikisha waje bila hofu yoyote na wafugaji watapata malisho ya uhakika kwa mifugo, watalima, watafanya biashara na kuungana na wanakilindi kwa shughuli za maendeleo” amesisitiza Mhe. Mgaza.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilindi Mhe. Mwalimu Mohamed Kumbi, ameeleza kuwa ziara ya Madiwani hao katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na kujifunza shughuli za Uhifadhi na Utalii lakini wameona umuhimu wa wananchi wa Ngorongoro kuhama katika eneo hilo kutokana na sheria za uhifadhi kutowaruhusu kufanya shughuli za kilimo, biashara, ujenzi wa nyumba na kumiliki vyombo vya usafiri kwa hiari kama ilivyo kwa wananchi walio nje ya Hifadhi.
“Wananchi waje Kilindi tutawapokea, Serikali itawapa ardhi na watakuwa huru kufanya shughuli zao masaa 24 bila kupangiwa muda wa kurudi makwao kama wanavyobanwa na shughuli za Uhifadhi” amesema Mhe. Kumbi.
Mhe. Michael Ole Simbiyu Diwani kutoka kata Saunyi eneo litakalokuwa na mradi wa ujenzi wa nyumba hizo, amebainisha kuwa Serikali ya Wilaya inaendelea kuwaelimisha wananchi wa Kilindi kuhusu ujio wa wanangorongoro na wananchi hao wako tayari kushirikiana na wenzao katika shughuli za ufugaji, kilimo, biashara na shughuli za utamaduni.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Elibariki Bajuta amewapongeza Madiwani hao kwa uamuzi wa kutembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwashirikisha madiwani hao, uongozi wa Wilaya ya Kilindi na Mkoa pamoja na wananchi wao katika hatua zote za utekelezaji wa mradi wa kujenga nyumba 5,000 na miundombinu mingine ya kijamii kabla ya kuwahamisha wananchi katika eneo la Wilaya hiyo.
“Mradi huu wa awamu ya pili kwa asimilia 100 utatekelezwa eneo la Wilaya ya Kilindi, Serikali itaendelea kushirikisha uongozi wa Wilaya, Mkoa na wananchi wa Kilindi.
….Utekelezaji wa mradi huu utaenda sambamba na kupima maeneo ya wananchi watakaokutwa na mradi na kupewa hati, kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kama shule, barabara, zahanati, maji, umeme, majosho pamoja na minada ya mifugo.’ amefafanua Naibu Kamishna Bajuta.