Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 29 /5/2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji katika kipindi cha miezi mitatu.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imefanikiwa kuwasaidia Walimu kwa kusitisha makato ya asilimia 2% kuchangia Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) na Chama Cha Kuwalinda na Kutetea Haki za Walimu (CHAKUHAWATA).
Awali walimu hao waliwasilisha malalamiko yao TAKUKURU kwamba wamekuwa wakikatwa mishahara yao na kuchangia vyama viwili kinyume na kifungu Cha 61 (1) cha sheria ya ajira na mahusiano kazini namba sita ya mwaka 2004 ambacho kinampa mfanyakazi Mamlaka ya kutoa kibali makato yake yaelekezwe Chama Cha wafanyakazi anachoona kinamfaa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 29 /5/2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji katika kipindi cha miezi mitatu, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke Bw. Holle Makungu, amesema kuwa kifungu cha 61(1) kikisomeka pamoja na kanuni ya 37 ya kanuni ya sheria na ajira na mahusiano kazini za mwaka 2007 havikutafasiriwa vizuri na Watendaji wa Manispaa ya Temeke.
“Walimu ambao ni wanachama wa CWT na CHAKUHAWATA walikuwa wanakatwa mishahara yao, kwa kuzingatia kifungu cha saba sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11/2007 tulimshauri Mkurugenzi Mhe. Elihuruma Mabelya kuhusu kadhia hiyo, na alisitisha mara moja makato hakuwai kutoa maelekezo ya makato” amesema Makungu.
Katika hatua nyengine ameeleza kuwa wamefanikiwa kufatilia miradi ya maendeleo 10 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi billion 14 na kubaini baadhi ya miradi kuwa na mapungufu ikiwemo upotevu wa fedha za wananchi unaotokana na kubadilishwa kwa mawanda ya mradi.
Amesema kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa nyumba za Walimu Shule ya Sekondari ya Pembamnazi Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni zenye thamani ya Sh 114, 683, 972.
Makungu amesema kuwa baadhi ya miradi mingine ni ujenzi wa madarasa 20 Shule ya Sekondari Nzasa Kilungule, ujenzi wa madarasa 32 Shule ya Sekondari Lumo, ufatiliaji wa miradi wa matumizi ya asilimia 10 unaofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
“Tumechukua hatua mbalimbali kwa wahusika ikiwemo kuwashauri, namna bora ya kutekeleza miradi ili kufikia malengo tarajiwa” amesema Bw. Makungu.
Hata hivyo TAKUKURU Temeke imefanya chambuzi za mifumo ikiwewa na lengo la kubaini mianya ya rushwa ambayo inaweza kupelekea vitendo vya rushwa kutokea nashauri Taasisi husika namna bora ya kurekebisha mapungufu yaliyobainika kwenye mifumo.
“Tumefanya uchambuzi za mfumo wa usimamizi wa mazao ya misitu na kubaini kukosekana kwa vizuizi katika Wilaya ya Kigamboni, pia wananchi hawana elimu ya kutosha ya sheria zinazohusika katika kutunza na kuvuna mazao ya misitu au miti iliyopo katika maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa” amesema Makungu.
Pia meeleza kuwa kupitia program ya TAKUKURU Rafiki iliyoundwa kwa lengo la kumfikia kila Mwananchi katika kata ambapo imeendelea kuibua kero kwa kushirikiana na wadau husika kwenye sekta mbalimbali.
Makungu amesema kuwa pamoja na kuendelea na juhudi za Kuzuia rushwa na kutoa elimu kwa umma bado kuna baadhi ya wananchi wachache ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu wamepokea malalamiko 54 , huku 46 yanahusiana na rushwa na 8 yasiyohusu rushwa.
“Malalamiko ya kuhusu rushwa tuliyopokea katika sekta ya Mahakama, Jeshi la Polisi, kilimo, TRA pamoja na sekta binafsi na zote tumechukua hatua kwa mujibu wa sheria” amesema Makungu.
Amesema kuwa wamefanikiwa kufungua kesi nne mahakamani, huku kesi mbili zimeamuliwa na mbili Jamhuri wamefanikiwa kushinda.
Makungu amesema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Temeke inaendelea kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma za jamii na utekelezaji wa miradi.
“Natoa wito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa ripoti kuhusu vitendo vya rushwa” amesema Makungu.