Na Abby Nkungu, Singida
SUALA la kuwalinda watoto wa kike walio chini ya
miaka minane dhidi ya ukeketaji bado ni changamoto katika Wilaya ya Singida baada ya wazazi na walezi kubuni
mbinu mpya ya kutekeleza mila hiyo potofu.
Joshua Ntandu ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali
la ESTL linalotekeleza mradi wa kupinga
ukatili na mila potofu ya ukeketaji
dhidi ya watoto wa kike katika wilaya hiyo anasema utafiti wa hivi karibuni
unaonesha wazazi na walezi wamebuni mbinu mpya ya kuwasugua sehemu za siri
watoto wachanga kwa kutumia ndulele, masizi, majivu au kuwafinya kwa kucha.
“Baada ya kusimamiwa vyema kwa sheria ya
kujamiiana inayotaja ukeketaji kuwa kosa la jinai na baadhi ya ngariba kufungwa
na mashirika mengi kuingia kwenye mapambano dhidi ya mila hiyo, cha kushangaza
baadhi ya wazazi na walezi ambao ndio wenye jukumu la kuangalia ulinzi na
usalama wa mtoto wameanza kukeketa kwa siri zaidi ili kukwepa sheria” alisema.
Alieleza kuwa utafiti wa Shirika hilo unaonesha
kuwa mjamzito anapokaribia kujifungua huomba ruhusa kwa mumewe kwenda
kujitizamia kwa bibi au shangazi ambako ukeketaji huo hufanyika muda mfupi
baada ya mtoto kuzaliwa.
Alisema kuwa bado jamii ya Vijijini inakumbatia
mila hiyo kwa kuamini kuwa mtoto asiyekeketwa anakuwa na mkosi katika familia
yake, ataendekeza umalaya akiwa mkubwa na anaweza kukumbwa na ugonjwa maarufu
kwa jina la kienyeji kamaa ‘lawalawa’ ambao hudhoofisha na kusababisha kifo.
“Kuna hii Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya miaka mitano kuanzia
2021/22 – 2025/26. Imekuja na masuala mtambuka ya afya, lishe bora, elimu,
ulinzi na usalama, nadhani ikisimamiwa vyema kwa kushirikiana nasi wadau wa
NGO’s tunaweza kuwa mwarobaini wa hili tatizo kwa kupiga kelele na kuokoa
watoto hawa wa miaka 0 hadi 8 wasifanyiwe ukatili huu” alisema na kuongeza kuwa
ushirikiano ndio nguzo kuu.
Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya Wanawake na
Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani
anakiri kuwa ukeketaji kwa watoto wachanga umeshika kasi.
“Kutokana na vichanga hao kuletwa kwenye
Vituo vya kutolea huduma ya afya kwa ajili ya kupatiwa huduma mbalimbali,
tumebaini jambo hilo ovu na la kikatili wakati wa utendaji wetu wa kazi”
alieleza Dk Muttani huku akikanusha kuwepo ugonjwa wa ‘lawalawa’ kwa watoto,
wasichana wala wanawake.
“Kinachofanyika ni kisingizio tu cha jamii
ili kutekeleza mila hiyo potofu. Kwa kweli, mila hii ya ukeketaji ni kikwazo
cha utekelezaji wa dhana ya ulinzi na
usalama wa mtoto mkoani Singida kutokana na athari za kiafya na kisaikosojia
kwa watoto kwa muda mrefu na muda mfupi” alisema.
Alitaja athari hizo kuwa ni kutokwa na damu
nyingi sehemu za siri au wakati mwingine husababisha kifo na maambukizi ya
virusi vya Ukimwi, Magonjwa ya kuambukiza ya mara kwa mara yanayoweza kumfanya
mtoto kuwa tasa anapofikia ukubwani, uharibifu wa mfumo wa njia ya uzazi,
matatizo wakati wa kujifungua na kutofurahia tendo la ndoa wakati wa kujamiana.
Hata hivyo, baadhi ya wazazi na walezi wanasema
pamoja na kutumia sheria kuwabana wanaoendeleza mila hiyo bado kuna haja ya
kuendelea kutoa elimu zaidi juu ya madhara ya ukeketaji kiafya.
“Hii ni mila, ni imani ya watu na imekaa kwenye
mioyo yao, haiwezi kutoka kirahisi hasa kwa jamii ya vijijini; hivyo ipo haja
ya elimu zaidi” anasema Ruth Daniel mkazi wa Mgori Singida Vijijini na kuungwa
mkono na Patrick Mdachi wa Singida mjini
ambaye anashauri Serikali iwawezeshe
ngariba kupata kipato mbadala kama mikopo ya vikundi ili waache
kutegemea ukeketaji.
Tanzania imedhamiria kukomesha kabisa ukatili wa
aina zote dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo ukeketaji kama sehemu ya
utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo
Endelevu 2030.