Na WAF- DODOMA
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa wanaume kushiriki katika masuala ya hedhi salama ili kuongeza kasi ya kuwalinda mabinti na wanawake dhidi ya magonjwa na kuwaongezea hali ya kujiamini katika jamii.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Mei 28, 2023 katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya hedhi salama Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu ya “Hedhi ni tunu na msingi wa afya kwa wasichana na wanawake, tuiwezeshe.”
“Watoto wa kiume na wababa wa kesho na marafiki wakubwa wa baba ni watoto wa kike, kwahiyo lazima tujue matatizo hao na tujue namna gani ya kuwasaidia, yani baba akielewa suluhu inakuwa rahusi sana.” Amesema Dkt. Mollel.
Amesema, suala la hedhi salama ni jambo la jamii yote, hivyo suala la uhamasishaji ni lazima liyaguse makundi yote ikiwemo kundi la watoto wakiume, kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwaweka salama mabinti na wanawake wote katika jamii.
Aidha, Dkt. Mollel ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuwezesha upatikanaji wa taulo za kike zaidi ya milioni tano kila mwaka kupitia jukwaa la hedhi salama ili kuwasaidia mabinti mbalimbali hasa wanaosoma katika maeneo ya vijini.
Nae, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Ahmed Makuwani amesema, changamoto ya hedhi inaonekana, hasa kwa kundi la vijana ambao wengi wako mashuleni ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya vyoo bora vyenye sehemu ya kunawa mikono na vyumba vya kubadilishia taulo za kike zilizo tumika, kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama kwenye vyoo vya taasisi na maeneo ya umma pamoja na kupata miundombinu ya kuteketeza taulo za kike zilizotumika.
Ameendelea kusema, Serikali kupitia Wizara ya Afya Serikali imeendelea kuweka mikakati mizuri kwaajili ya hedhi salama ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa taulo, upatikanaji wa maji safi na kuwa na vyumba vyenye usiri.