Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha mbunge wa zamani wa Butiama na Musoma Vijijini, Wakili Nimrod Mkono alipowaongoza waombolezaji kuaga mwili wa Wakili huyo kwenye viwanja vya Karimjee Mkoani Dar es salaam, Mei 28, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
aziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipowaongoza waombolezaji kuaga mwili wa mbunge wa zamani wa Butiama na Musoma Vijijini, Wakili Nimrod Mkono kwenye viwanja vya Karimjee mkoani Dar es salaam, Mei 28, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa mbunge wa zamani wa Butiama na Musoma Vijijini, Wakili Nimrod Mkono kwenye viwanja vya Karimjee mkoani Dar es salaam, Mei 28, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya viongozi walioshiriki kuaga mwili wa Mbunge wa zamani wa Butiama na Msoma Vijijini, Wakili Nimrod Mkono kwenye viwanja vya Karimjee mkoani Dar es salaam, Mei 28, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole, Mary Mkono, mjane wa mbunge wa zamani wa Butiama na Musoma Vijijini, Nimrod Mkono wakati alipowaongoza waombolezaji kuaga mwili wa Wakili na Mwansiasa huyo kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es salam, Mei 28, 2023. Wa pili kushoto ni, Bi. Deborah Nyakirang’ani. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
..……………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na aliyewahi kuwa Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Marehemu Wakili Nimroad Mkono na kwamba itaendelea kumuenzi kwa kazi nzuri alizofanya.
“Serikali imepoteza mtu muhimu, itaendelea kutambua mchango alioutoa na itaendelea kuyaenzi yale yote mema aliyoyafanya enzi za uhai wake. Wananchi kila mmoja kwa imani yake tuendelee kumuombea.”
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 28, 2023) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika shughuli ya kumuaga marehemu Wakili Nimrod Mkono iliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee, Jijini Dar es Salaam.
Amesema enzi za uhai wake marehemu Wakili Mkono alikuwa mtumishi mwema na mshauri mzuri kwa Serikali hususani katika sekta ya sheria pamoja na kuishauri namna bora ya kutunga sheria na kanuni zake kupitia Bunge.
Waziri Mkuu amesema mbali na mchango mkubwa alioutoa katika masuala ya kisheria pia, marehemu aliisaidia Serikali kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule na afya kupitia fedha zake binafsi.
Naye, Dkt. Harisson Mwakyembe akimzungumzia marehemu amesema Wakili Mkono alikuwa ni taasisi katika uwakili kutokana na ubunifu mkubwa aliokuwa nao katika kukuza huduma za kisheria na ameacha alama kubwa.
Kwa upande wake, mdogo wa marehemu, Bw. Shadrack Mkono akisoma wasifu amesema Wakili Mkono alizaliwa Agosti 18, 1943 katika kijiji cha Busegwe Kata ya Busegwe na anatarajiwa kuzikwa Mei 29 kijijini Kigori wilayani Butiama mkoani Mara. Wakili Mkono alifariki Aprili 18, 2023 nchini Marekani alikokuwa akipatiwa matibabu.