NA VICTOR MAKINDA: MOROGORO
Jumuiya ya Kikristu Tanzania (CCT) Mkoa wa Morogoro imesema kuwa inaridhishwa na utendaji wa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa imekuwa muarobaini wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Jumuiya CCT mkoa wa Morogoro, Mchungaji Regnard Mdugo, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa bonanza la michezo lililowakutanisha viongozi wa dini kutoka madhehebu mbali mbali ya kikristu, lililofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa mjini Morogoro ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya CCT.Mchungaji Mdugo alisema kuwa kasi ya utendaji wa Rais Samia katika kushughulikia changamoto za wananchi kwenye maeneo muhimu ya elimu, afya, miundombinu na maji inakata kiu ya watanzania.“Jumuiya ya Kikristu (CCT)
Mkoa wa Morogoro, inaridhishwa na kasi ya utendaji wa Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na tunaukiri ukweli kuwa anafanya kazi nzuri sana katika uongozi wake kwa kuwa amejikita katika kushughulikia matatizo ya wananachi kwa kuimarisha sekta za elimu, maji, afya na miundombinu”. Alisema Mchungaji
Mdugo.Aliongeza kusema kuwa hakuna ubaya kwa viongozi wa dini kusifu viongozi wa kisiasa pindi wanapoitendea vizuri jamii wanayoiongoza na vivyo hivyo ni kazi ya viongozi wa dini kukosoa ikiwa kukabainika mwenendo usioridhisha.
Mchungaji Mdugo alisema kazi ya viongozi wa dini ni kuhubiri upendo na amani lakini kazi hiyo hushindwa kufanikiwa ikiwa viongozi wa kisiasa wataenenda kinyume na matakwa ya watu.“ Kunapokuwa na kiongozi mcha Mungu, mwenye kuguswa na kutatua matatizo ya watu wake, kiongozi huyo huturahisishia kazi ya kuhubiri amani sisi viongozi wa dini kwa kuwa watu wakiwa na njaa na mahangaiko somo la amani huwa ni gumu.” Alisema.
Aliongeza kusema kuwa Rais Samia tangu ameshika hatamu za uongozi wa nchi, amejitahidi sana kuhakikisha Tanzania inakuwa na maridhiano baina ya vyama vya siasa, amani, umoja na mshikamano wa jamii huku akitia nguvu kutatua changamoto za wananchi hatua ambayo inapaswa kupongezwa na kila mwenye dhamira njema.