Magari na pikipiki zilizotolewa na Benki yamaendeleo ya Ujerumani(KFW) kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi na ulinzi wa maliasili katika wilaya ya Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas kushoto,akipokea funguo za magari manne na pikipiki 15 kutoka kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Adrehem Nziku,magari na pikipiki hizo zinakwenda kusaidia katika ulinzi wa maliasili na kuendeleza shughuli za utalii mkoani Ruvuma,kulia Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya na wa pili kulia Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya Tunduru Ngollo Malenya akionyesha juu funguo za magari yatakayotumika kuimarisha sekta ya utalii ya uhifadhi wa maliasili katika wilaya hizo,magari hayo yametolewa na Benki ya maendeleo ya Ujerumani,kushoto Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas na kulia mwakilishi wa katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Adrehem Nziku.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya akikabidhi funguo za magari mawili na pikipiki kwa kati bu tawala wa wilaya hiyo Aden Nchimbi yaliyotolewa na Serikali ya Ujeruman ili kuendeleza utalii na kuhifadhi maliasili wilayani humo,kulia Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Namtumbo Juma Pandu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Hemed Hairu Mussa akijaribu kuendesha moja kati ya pikipiki zilizotolewa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya maendeleo ya nchi hiyo(KFW)ili kusaidia kuendeleza sekta ya utalii na uhifadhi wa maliasili,anayeshuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Marando.
……………………………..
Na Muhidin Amri, Songea
WIZARA ya maliasili na utalii, imekabidhi magari manne na pikipiki kumi na tano kwa Serikali ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kuboresha ulinzi na uhifadhi wa maliasili katika mfumo wa Ikolojia wa Selous.
Akikabidhi magari na pikipiki hizo kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Adrehem Nziku amesema,vitendea kazi hivyo vimetolewa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya maendeleo ya Ujerumani (KFW).
Amesema,Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali ya Ujerumani katika kuhifadhi maliasili ya nchi yetu kwa maslahi mapana ya Watanzania na Dunia kwa ujumla.
Amesema kuwa,juhudi hizi zinaonekana kwa vitendo kwani takwimu za sasa zinaonyesha kuwa takribani robo ya eneo la Tanzania(kilomita za mraba zipatazo 300,000)limehifadhiwa.
Amesema,vitendea kazi hivyo vilivyonunuliwa kupitia mradi wa SECAD kama sehemu ya utekelezaji wa mradi kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ulinzi na uhifadhi katika ushoroba wa Selous-Niassa zitakwenda kupunguza uhaba wa vitendea kazi katika katika wilaya ya Namtumbo na Tunduru.
Ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa ufadhili wa fedha kiasi cha Euro milioni 18 zilizotolewa kwa ajili ya kuendelea kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa maliasili katika mfumo wa Ikolojia wa Selous kupitia mradi wa SECAD.
Aidha,amewapongeza wadau wa uhifadhi( shirika la FZS na WWF)wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi wa SECAD ambao kwa pamoja wamechangia jumla ya Euro 146,000,00 katika gharama za kutekeleza mradi.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake makubwa na kutoa fursa kwa wawekezaji wa nyanja mbalimbali kuja kuwekeza katika nchi yetu.
Amesema,bila maono yake ya kufungua njia na kusimamia huwenda tusingepata matokeo ya uwekezaji hasa katika sekta ya utalii kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa ambapo Watanzania na Dunia wanaendelea kushuhudia watalii kutoka mataifa mbalimbali wakifika hapa nchini.
Ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya maendeleo ya nchi hiyo(KFW),kutoa magari na pikipiki na wadau shirika la WWF kwa kazi kubwa inayofanya katika kuhakikisha uhifadhi unaendelea kuwepo na kuimarisha mahusiano kati ya wahifadhi na wananchi.
Kwa mujibu wa Kanal Laban,kumekuwa na tatizo kubwa la wanyama wakali na waharibifu katika wilaya ya Namtumbo na Tunduru ambapo kwa muda wa miaka mitatu zaidi ya wananchi ya 24 wameuawa kwa kukanyagwa na Tembo na wengine 21 kujeruhiwa.
Kanal Laban,ametoa wito kwa wizara ya maliasili na utalii na wadau wengine,kusaidia katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili zetu ili ziendelee kutumika kuongeza pato na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mkuu wa mkoa,ameagiza magari na pikipiki hizo zinatakwenda kutumika kupunguza matukio ya wanyama wakali na waharibifu na kunusuru maisha ya wananchi katika wilaya hizo mbili na siyo vinginevyo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Benki ya maendeleo ya Ujerumani Francis Rusengulla amesema, hadi sasa Bebki hiyo imewekeza zaidi ya Euro 100( Sh.bilioni 25) katika uhifadhi nchii Tanzania.
Amesema,KFW imejikita sana katika sekta ya bioanuwai,ulinzi wa maliasili na kutoa ruzuku kwa mahitaji ya dharura ndani na nje ya hifadhi za wanyamapori ambapo wakati wa janga la Corona 2020 Serikali ya Ujerumani kupitia KFW ilitoa jumla ya Sh.bilioni 89 za dharura ili kuimarisha uhifadhi hapa nchini.
Pia wametoa mitambo ya kutengeneza barabara,malori ya kubebea mafuta,maji na vifusi pamoja na kujenga vituo vya doria na nyumba za watumishi na ukumbi wa chakula na vyumba vya madarasa shule ya Sekondari Likuyusekamaganga.