Naibu Gavana wa BoT, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, akizungumza katika mkutano wa wadau wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere uliofanyika katika kumbi za mikutano za BoT Dar es Salaam.Mwakilishi wa Familia ya Mwl. Julius K. Nyerere katika Bodi ya Wadhamini ya mfuko huo, Bw. Madaraka Nyerere, akizungumza katika mkutano wa wadau wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere uliofanyika katika kumbi za mikutano za BoT Dar es Salaam.
Wadau wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere katika mkutano uliofanyika katika kumbi za mikutano za BoT Dar es Salaam.
Naibu Gavana wa BoT, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, katika picha ya pamoja na wanufaika waliohitimu masomo chini ya ufadhili wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere.
Naibu Gavana wa BoT, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, katika picha ya pamoja na wanufaika wanaoendelea na masomo chini ya ufadhili wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere.
………………………………
Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere ulioanza kutoa ufadhali katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/14 umeendelea kuongeza hamasa na ufaulu kwa wanafunzi wa kike katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika masomo ya Hisabati na Sayansi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano uliokutanisha wadau wa mfuko huo uliofanyika katika kumbi za mikutano za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam, Naibu Gavana, Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, alisema kuwa mpaka sasa mfuko huo umetoa udhamini kwa jumla ya wanafunzi wenye ufaulu wa juu 72, ambapo kati ya hao 50 ni wanawake na 22 ni wanaume.
“Mafanikio haya yanaendana na lengo la mfuko la kuongeza ufaulu wa wanafunzi hasa wa kike katika masomo ya Sayansi na Hisabati. Haya ni mafanikio makubwa ya mfuko katika kuleta usawa wa kijinsia katika maeneo hayo nchini,” alisema Dkt. Kayandabila.
Aliongeza kuwa mkutano huo unatoa fursa ya kujuana, kubadilishana uzoefu katika mambo mbalimbali na kupata ushauri toka uongozi wa mfuko na BoT. “Mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wa mfuko kujadilianakwa pamoja jinsi ya kuongeza ushirikiano kati yao, mfuko na Benki kuu ya Tanzania kwa ujumla,” alisema.
Naye Mwakilishi wa Familia ya Mwl. Julius K. Nyerere katika Bodi ya Wadhamini ya mfuko huo, Bw. Madaraka Nyerere, aliwaasa wanufaika kumuenzi Mwl. Nyerere kwa kutumia elimu waliyopata chini ya udhamini wa mfuko huo kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii inayowazunguka.
Mkutano huo umewakutanisha wadau wote muhimu wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, wakiwemo wajumbe ya Bodi ya Wadhamini wa Mfuko, Kamati na Wanufaika wa ufadhali wa mfuko ikiwemo wahitimu na wanoendelea na masomo ndani na nje ya nchi.