Ujumbe wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Saidi Yakubu wamekutana na kufanya kikao cha pamoja na Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni ya Afrika Kusini na kubadilishana uzoefu ili kuboresha sekta hizo na kuwaletea maendeleo wananchi wa pande zote mbili.
Kikao hicho kimefanyika Mei 26, 2023 katika ofisi za Wizara ya Michezo. Sanaa na Utamaduni ya Afrika Kusini jijini Pretoria ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo kwa ujumbe huo kutoka Tanzania.
Akiongea katika kikao hicho Katibu Mkuu Bw. Yakubu amewajulisha kuwa Tanzania, Uganda na Kenya kwa pamoja wanaratibu kwa pamoja michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Afcon) 2027 na kuwaomba kuunga mkono juhudi hizo za Afrika Mahariki kuandaa mashindano hayo.
Kwa upande wa Afrika Kusini wamesema linapokuja suala la ushirikiano, Afrika Kusini ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kuwa udugo baina ya nchi hizo mbili ni wa kihistoria ambao umeasisiwa na viongozi Mwal. Julius MNyerere wa Tanzania na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.
Aidha, pande zote mbili zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo Novemba 17- Desemba 04, 2022 umekuwa mwendelezo wa uhusiano mwema kwa kuja na namna mpya ya ushirikiano kwa kuanzisha Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania, tamasha lililohusisha mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Pwani na Dodoma.