Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Maharage Chande akiunguma wakati alipokutana na wahariri wa vyombo vya ahbari kwenye hoteli ya Serena jana.
…………………………………..
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linaendelea na jitihada za kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme kwa ajili ya kufikia lengo la uhitaji wa umeme ili kuendelea kukuza uchumi.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Maharage Chande, amesema kuwa kwa mujibu wa tafiti ili kukuza uchumi, idadi ya watu milioni moja wanahitaji umeme megawati 1,000.
Bw. Chande amesema kuwa kwa Tanzania kwenye idadi ya watu milioni 60 hivyo wanahitaji megawatt 60,000.
“Kwa sasa tuna umeme megawati 1,800 na imeongezeka asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2022, kwani tulikuwa na megawati 1,600 na hadi kufikia mwaka 2024 tutakuwa na megawatt 3,800” amesema Bw.. Chande.
Amesema kuwa wanaendelea kutekeleza mipango kwa kuzingatia mpango wa Taifa, ilani ya Chama Cha Mapiduzi (CCM) katika kuhakikisha miradi yote ya umeme inakamilika na kuleta tija kwa Taifa.
Ameeleza kuwa miradi ya umeme iliyopo na inayokuja itasaidia kuzalisha umeme megawati 5,000 hadi kufikia mwaka 2025.
Bw. Chande ameeleza katika awamu ya kwanza iliyopita wametumia trillion 1.9 ambapo kuna miradi 29 ya usambazaji umeme ambayo inasaidia kuzuia mgao wa umeme.
“Tunaendelea kuzalisha umeme kupitia vituo vyetu vilivyopo nchini pamoja na kuongeza miradi mipya ili kuhakikisha tunafikia malengo” amesema Bw. Chande.